Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dk. Ashatu Kijaji (Mb).
Na Peter Haule, WFM,
Dodoma
Serikali imewaonya
wanaofanya biashara ya upatu (Pyramid Scheme) kwa kuwa sio halali na hakuna
taasisi wala mtu binafsi aliyepewa leseni ya kufanya biashara hiyo.
Onyo hilo limetolewa
bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu
Kijaji, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Munira Mustafa
Khatib, aliyetaka kujua ni lini Serikali itadhibiti biashara za upatu ambazo
zimekuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Taifa.
Dkt. Kijaji alisema
kuwa, kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, biashara ya upatu ni
haramu na huendeshwa kinyume na sheria na taratibu za nchi hivyo Serikali
huchukua hatua dhidi ya wahusika kama ilivyofanya kwa taasisi ya DECI.
“Washiriki wa
biashara ya upatu na wale wanaoshawishi ufanyaji wa biashara hiyo, wote
wanatenda kosa na wanatakiwa kupata adhabu na sio kusaidiwa na Serikali”,
alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa Serikali
itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya biashara ya upatu na tayari
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na na Mamlaka ya Masoko ya
Mitaji na Dhamana (CMSA), ilitoa taarifa kwa umma kuhusu madhara hayo na
kuwahimiza wananchi kutoa taarifa ya watu au taasisi inayofanya biashara hiyo.
Dkt. Kijaji alisema
kuwa, kwa kuwa waathirika wakubwa wa biashara hiyo ni vijana na wanawake,
Serikali kupitia Bunge, mwaka 2018, ilipitisha mabadiliko ya sheria ya fedha
ambapo asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri yanatakiwa
kutolewa kama mikopo isiyo na riba kwa kundi hilo.
Alisema Wizara ya
Fedha na Mipango kuna Taasisi ya huduma ndogo ya fedha-SELF, ambayo
inatoa mikopo kwa kundi hilo kwa riba nafuu na inafanya vizuri katika maeneo
mengi nchini.
Amewataka Vijana na
wanawake kutojihusisha na biashara haramu bali watumie taasisi halali zinazotoa
riba nafuu na zenye lengo la kujenga uchumi wa Taifa.
No comments:
Post a Comment