HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 02, 2019

TEAM SAMATTA YAITAMBIA TENA TEAM KIBA, ABDUL KIBA AMKERA KAKA YAKE

NA SALUM MKANDEMBA

MSIMU wa pili wa Kampeni ya Nifuate inayoratibiwa na Taasisi ya SAMA-KIBA Foundation, umeunguruma Jumapili hii ya Juni 2 jijini Dar es Salaam, kwa pambano la soka baina ya marafiki wa Mbwana Samatta na Ali Kiba ‘Team Samatta’ dhidi ya ‘Team Kiba.’ 
 
Kwa mara ya pili mfululizo, Team Kiba imeshindwa kufurukuta mbele ya Team Samatta, baada ya kukubali kipigo cha mabao 6-3, mwaka mmoja tangu ilipochapwa mabao 4-2 katika msimu wa kwanza wa Kampeni hiyo ya kuchangia Sekta ya Elimu na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Nifuate ni kampeni inayolenga kukusanya fedha kwa ajili ya kusapoti elimu na watoto wanaoishi katika vituo vya yatima, wanaoishi katika mazingira magumu na wenye uhitaji, kampeni inayoratibiwa na SAMA-KIBA Foundation, taasisi ya ushirika ya mastaa hao.

Katika pambano la Jumapili hii, Team Samatta imeibuka na ushindi huo mnono kupitia mabao ya Hassan Kessy (kwa penalti), Samatta mwenyewe (mawili), Thomas Ulimwengu, Kelvin John na Shaaban Idd Chilunda, huku mabao ya Team Kiba yakifungwa na Simon Msuva (mawili) na Meddie Kagere.

Kulikuwa na burudani kali ya soka kutoka kwa nyota wakongwe, wa umri wa kati na chipukizi, huku Abdul Kiba aliyeingia kuchukua nafasi ya kaka yake aliyeumia, aliweka rekodi ya kukosa penalti mbili ndani ya dakika mbili za mwisho, kosa kosa zilizomkera sana Ali Kiba akiwa nje ya uwanja.

Penalti hizo zilizoacha gumzo uwanjani hapo hata mitaani kwa wafuatiliaji kwa njia ya televisheni, zilitolewa na mwamuzi Othman Kazi, ya kwanza ikitokana na kuchezewa madhambi kwa mmoja wa washambuliaji wa Team Kiba, ambako Abdul Kiba alipiga na kipa wa Team Samatta, Kabari Faraji alipangua.

Baada ya Kabari aliyeingia kuchukua nafasi ya Juma Kaseja kupangua, ikawa kona, ambayo ilipopigwa, Mwinyi Kazimo wa Team Samata aliunawa mpira hu na Mwamuzi Kazi kuamuru ipigwe penalti, ambako Abdul Kiba akakosa tena. Ali Kiba akiwa nje, alionekana kujirusha kwa hasira mara zote mdogo wake alipopoteza.

Katika mechi hiyo, Team Samatta iliundwa na Juma Kaseja, Jerry Santo, Hassan Kessy, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Haruna Moshi ‘Boban,’ Mrisho Ngassa, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta, Farid Mussa na Issa Rashid.

Kelvin John, Mohmmed Samatta, Athuman Idd ‘Chuji,’ Amri Kiemba, Shaaban Idd Chilunda, Kabari Farji, Alex Massawe na Mwinyi Kazimoto wakiingia kwa nyakati tofauti wakitokea benchi, kutoa mchango wao katika pambano hilo.

Kikosi cha Team Kiba ambacho kilifanya mabadiliko machache, kiliundwa na Aishi Manula, Juma Abdul, Pascal Wawa, Aggrey Morris, Said Ndemla, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Ali Kiba, Meddiee Kagere na Shiza Kichuya.

Wakali kama Abdul Kiba, Feisal Salum ‘Fei Toto,’ Abdi Banda, Stanley Nkomola, James Msuva, Khalid Tunda ‘Tunda Man,’ waliingia wakitokea benchi, ambako Tunda Man mkali wa Bongo Fleva alichukua nafai ya Manula golini na kuzuia michomo kadhaa kwa ustadi mkubwa.

No comments:

Post a Comment

Pages