HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 02, 2019

Wataalam wa Biotekinolojia watakiwa kushirikiana na COSTECH, Serikali

 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi (COSTECH), Dk. Amos Nungu, akizungumza na wanasayansi (hawapo pichani) kuhusu wanasayansi hao kushirikiana na tume hiyo kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Maurilio Kipanyula.
Mratibu wa Biotekinolojia na Usalama wa Chakula COSTECH, Dk. Beatrice Lyimo, akielezea majukumu ya Idara yake kwa wanasayansi watafiti. 
Wanasayansi wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi Teknolojia COSTECH Dk Amos Nungu (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Teknolojia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Maurilio Kipanyula.


NA SULEIMAN MSUYA

WANASAYANSI wa masuala ya Biotekinolojia nchini wametakiwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ili kuendelezea teknolojia hiyo ambayo ni mpya nchini.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu, wakati wa mahojiano ya mwandishi na wanasayansi mkoani Morogoro.

Alisema COSTECH ipo tayari kushirikiana na wanasayansi hao wa masuala ya Biotekinolojia nchini kuhakikisha tafiti zao zinakuwa na matokeo chanya kwa jamii.

Dk. Nungu alisema pia COSTECH imekuwa ikiendeleza wabunifu mbalimbali ambao wanabuni vitu vyenye matokeo chanya kwa jamii.

"Tumekuwa tukiwezesha taasisi, watafiti na wabunifu mbalimbali hivyo sisi tupo wazi kwa nyie wanasayansi kuja na maandiko yenu na tutayafanyia kazi kulingana na fedha zilizopo, msisubiri mpaka tutangaze," alisema.

Mkurugenzi huyo wa COSTECH alisema iwapo kada hiyo ya wanasayansi hasa wa masuala ya Biotekinolojia watapata nafasi ya kuonesha tafiti zao ni wazi dhana ya nchi kufikia uchumi wa kati itafanikiwa.

Alisema tume itahakisha tafiti hizo zinafika Serikalini kirahisi na kufanyiwa kazi kwa maslahi ya nchi na wananchi.

Aidha, Dk. Nungu amewashauri wanasayansi kutumia lugha ambayo inaeleweka kwa waandishi wa habari ili kurahisisha kutoa taarifa sahihi kuhusu tafiti zao Biotekinolojia.

Alisema wapo wanasayansi ambao wanatumia lugha za kisayansi hali ambayo inakwamisha mwandishi na jamii kushindwa kuelewana.

Dk. Nungu alisema pia wanasayansi wanapaswa kuandaa taarifa za tafiti zao kwa ufupi ili watoa maamuzi waweze kuelewa na kuchukua uamuzi.

"Niwaomba ndugu zangu wanasayansi mnapoandaa taarifa za tafiti zenu zingatieni lugha ambayo ni rahisi kueleweka kwani itasaidia jamii kupata ujumbe sahihi," alisema Dk. Nungu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu (STI), Profesa Maurilio Kipanyala alisema Serikali kupitia idara hiyo imedhamiria kuendeleza teknolojia nchini ikiwemo Biotekinolojia.

Alisema serikali imekuwa ikishirikiana na taasisi kama COSTECH, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikukuu cha Mbeya (MUST), Chuo Kikuu cha Nelson Mandeka na Tume ya Mionzi Tanzania.

"Sisi dhana hii tunaitekeleza katika dhana ya STI lakini pia Biotekinolojia ipo ndani kinachohitajika ni kuondoa wigo uliopo kati ya pande husika," alisema.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa fedha za utafiti kwa COSTECH ambapo kwa mwaka wa fedha 2018/19 ilitengewa Sh.Bilioni 8.6 na mwaka unaokuja 2019/20 wametengewa Sh.Bilioni 6.7.

Alisisitiza uandaaji wa taarifa kwa ufupi ili kujenga hoja kwa watoa maauzi waeeze kuongeza bajeti ili tafiti zifanyike.

Prof. Kipanyula alisema uwekezaji wa fedha katika tafiti unahitaji kupata matokeo ambayo yatamaliza changamoto za jamii.

Mkurugenzi huyo alisema idara itahitaji kupata taarifa kuhusu masuala ya Biotekinolojia ili kuangalia kuwa inaendana na sera ya serikali katika eneo hilo.

"Ushirikiano ndio njia sahihi ya kufanya kazi hasa hizi za utafiti ni imani yangu nyie kama wanasayansi mtazingatia hilo na Biotekinolojia itasambaa kila mahali," aliongeza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanasayansi watafiti kutoka vyuo mbalimbali nchini walisema iwapo tafiti zao zikitekelezwa ni dhahiri Tanzania ya uchumi wa kati itafikiwa.

Baadhi ya wanasayansi hao ni Dk. Miccah Seith wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk.Charles Lyimo wa SUA, Dk.Siana Nkya wa Chuo Kikukuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE) na Dk.Daniel Maeda wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Wanasayansi hao wamesema maendeleo amabayo yanaonekana duniani kwa sasa asilimia kubwa yamejikita kwenye Biotekinolojia hivyo Tanzania inapaswa kuwekeza eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages