HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 02, 2019

VURUGU ZAFUTA MECHI ZA ‘PLAY OFF’ PAMBA VS KAGERA, GEITA GOLD VS MWADUI FC

NA SALUM MKANDEMBA

MKANGANYIKO umegubika mechi za mtoano ‘play off’ ya kuwania kupanda ama kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), kiasi cha kulilazimisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuahirisha mechi hizo kati ya Pamba SC na Kagera Sugar FC, na Geita Gold FC na Mwadui FC.

Pamba SC na Geita Gold zimepata nafasi hiyo baada ya kushinda ‘play off’ iliyozihusisha timu za Daraja la Kwanza, huku Kagera Sugar na Mwadui FC zikilazimika kupigania kubaki Ligi Kuu Tanzania kwa kushinda mechi hizo, baada ya kumaliza nafasi za 18 na 17 katika TPL 2018/19.

Washindi wa jumla wa mechi hizo mbili, watapata nafasi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL 2019/20). Kiini cha mgogoro uliosababisha mechi kuahirishwa ni madai ya Geita Gold na Pamba kudai kulipwa pesa za haki za televisheni, kwani Aza Tv inazilipa timu za Ligi Kuu.

Mechi hizo zilizokuwa zichezwe Jumapili ya Juni 2, zimesogezwa mbele hadi kesho Jumatatu ya Juni 3, huku taarifa ya TFF kupitia Ofisa Habari wae Cliford Ndimbo, ikisema imefanya hivyo kutokana na sababu za kiusalama baada ya kuwepo kwa tishio la vurugu. 

“Mechi zote, zikiwemo za marudiano zitakazochezwa Juni 8 zitaoneshwa moja kwa moja ‘live’ na kituo cha televisheni cha Azam. Zimeahirishwa kwa sababu usalama wa magari ya Azam TV ulikuwa mdogo kutokana na baadhi ya washabiki kutishia kuvunja vioo wakipinga mechi hizo kuoneshwa. 

“Kwa mujibu wa kanuni za Ligi, haki za matangazo ya televisheni ni mali ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Timu itakayozuia mechi yake kuoneshwa, itahesabika kuwa haikufika uwanjani, hivyo itachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni,” imesema taarifa ya TFF. 

Taarifa hiyo imeongeza kwa kuwataka viongozi wa timu husika kupuke kutoa matamko ambayo ni kinyume na kanuni za mpira wa miguu na kuonya kuwa watakaokwenda kinyume na angalizo hilo, watachukuliwa hatua za kinidhamu na kimaadili.

No comments:

Post a Comment

Pages