Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres
Magiri akifungua jana mkutano wa siku moja wa wadau wa sekta ya tumbaku
wilayani humo. (Picha na Tiganya Vincent).
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa
wadau wa sekta ya tumbaku wilayani Sikonge wakisikiliza jana hotuba ya ufunguzi
ya Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri (hayupo katika picha).
NA TIGANYA VINCENT
VIONGOZI wa Vyama vya Msingi vya
Ushirika (AMCOS) wilayani Sikonge wametakiwa kuingia mikataba ya kisheria na wanachama wao ili
kuwabana wasitoroshe tumbaku na kusababishia deni.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri wakati akifungua
mkutano wa siku moja wa wadau wa sekta ya tumbaku ambao uliwahusisha Madiwani ,
Viongozi wa AMCOS na Wawakilishi kutoka Kampuni za ununuzi wa tumbaku.
Mkuu
huyo wa Wilaya ya Sikonge alisema
hatua hiyo itasaidia kuuwachukulia hatua za kisheria viongozi na wanachama
wanaobainika kukiuka taratibu za vyama ikiwemo kutorosha tumbaku na kuuza kwa njia ya magendo.
Magiri
aliongeza kuwa vitendo vya namna hiyo vimesababisha baadhi ya AMCOS kufa kwa
sababu ya kuwa na madeni na kushindwa kupata makisio ya kilimo cha tumbaku.
Aidha
Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wanunuzi wa tumbaku kuhakikisha wanafanya mapema
malipo ya wakulima ili kuepuka utoroshaji wa tumbaku kwa ajili ya kutafuta
fedha za haraka za kusaidia familia zao.
Magiri
alizitaka Benki kuidhinisha mikopo ya vyama vya msingi kwa wakati ili
kumwezesha msambazaji kusambaza pembejeo kwa wakati.
Akisoma maazimio ya
mkutano huo kwa niaba ya wadau wa sekta ya tumbaku Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Sikonge Peter Mihayo
Nzalalila alisema wataandika barua kwenda kwa Waziri wa Kilimo
kuomba kuongezewa madaraja ya tumbaku kwa sababu uwepo wa madaraja machache umesababisha
mkulima kunyonywa.
Alisema wamekubaliana
kuwa Vyama vya msingi viwasaidie wakulima wao kujikomboa kiuchumi kwa kuwapa
makisio ambayo yapo ndani ya uwezo wao.
Nzalalila aliongeza Vitabu
vya sheria vya Bodi ya tumbaku vitafsiriwe katika lugha ya Kiswahili na
kugawiwa kwa viongozi wa vyama vya msingi ili viwasaidie wanachama wote kujua
haki zao za msingi.
Alisema kuwa ni vema mikopo
ya pembejeo itolewe mapema mwezi wa Tisa ili wakulima wajiandae mapema kuingia
kwenye msimu wa kilimo.
Nzalalila alisema kuwa makisio
ya wakulima wa kujitegemea pia yaingizwe kwenye takwimu za ushirika ili
wakulima hao wasikose pa kuiuzia tumbaku yao.
Awali akitoa kilio cha
wakulima wa tumbaku Mwenyekiti wa Kisanga AMCOS Rashid Mazinge alisema mauzo ya
msimu huu yamekuwa mabaya sana kwani wakulima wengi wameuza chini ya wastani wa
Dola moja jambo ambalo litasababisha wengi wao kulaza madeni ya pembejeo.
Alisema wateuzi wa
Kampuni wamekuwa wakitoa bei ya chini kwa kisingizio kuwa tumbaku ya mwaka huu
haina ubora.
Aidha Mazinge alisema
kuchelewa kwa mbolea kuwafikia wakulima wengi kumesababishia hasara kubwa
wakulima na kupata bei ya chini.
No comments:
Post a Comment