HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 03, 2019

VIZIWI WATAKA LUGHA YA ALAMA POLISI, MAHAKAMA NA MAGEREZA

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Walimu Viziwi Tanzania (CWUT)  kimelitaka Jeshi la Polisi,  Mahakama na Magereza kuweka utaratibu wa kujifunza lugha ya alama ili iweze kuwasaidia  kuelewana na kuhudumia jamii ya watu wenye ulemavu nchini hasa viziwi.

Chama hicho kimesema viziwi  wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali hasa ya kutoelewa na makundi hayo pindi wanapikamatwa au kuwa na kesi mahakamani kutokana na lugha ya alama kutotambulika.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Rais wa Chama hicho Theresia Nkwera wakati wa mkutano wa Viziwi uliokuwa ukijadili changamoto wanazokumbana nazo kutoka kwa vyombo vya dola na usalama  kutokana na kutokujulikana kwa lugha ya alama.

Alisema wanaiomba serikali itoe ushirikiano kwao kwa kuwawekea utaratibu Jeshi la Polisi, Mahakama na Magereza kujifunza lugha hiyo ya alama ili waweze kuwasiliana vizuri na watu wenye uhitaji hasa viziwi.

"Kutokuwepo kwa watu wanaofahamu lugha ya alama katika jeshi la Polisi, Mahakamani hata Magereza kumechangia viziwi wengi kuwekwa ndani bila sababu na wengine kufungwa kwa makosa wasiyoyafanya.

Ndio maana tunasisitiza kuwa ni muhimu kwa lugha hii ya alama ijulikane na makundi haya ili iwe rahisi kuwasiliana na sisi viziwi, jambo hili kama litafanikiwa basi tutakuwa tumewasaidia sana Viziwi na wao watajiona wanathamani kama binadamu wengine, "

Aidha alisema jamii ya viziwi pia wanakabiliwa na changamoto ya kutokujua sheria jambo ambalo amedai kuwa linapaswa kuangaliwa kwa ukarimu na kupatiwa ufumbuzi na wadau mbalimbali. 


Naye Mratibu wa Mradi wa Lugha ya alama kwa vyombo vya dola katika kujenga ushawishi na utambuzi wa sera na sheria za watu wenye ulemavu,  Francis Mbiso alisema mradi huo ambao unafadhiliwa na Foundation of Civil Society (FCS) unalengo la kuhamasisha vyombo hivyo vya dola kujifunza lugha ya alama.

Alisema  ni muhimu kwenye vyuo vya Magereza, Mahakama na Polisi kuweka utaratibu wa kufundisha lugha hiyo ili waweze kuwasaidia viziwi pindi wanapopata matatizo au kukamatwa kwa makosa mbalimbali.

"Tukikutana na wadau hao tutapitia sera zao na kama hazitakuwa na vikwazo basi tutawaeleza umuhimu wa kuchomeka lugha ya alama na titawahamaisha lugha hii itumike ili kurahisisha mawasiliano na viziwi waweze kupata haki, "alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages