HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 23, 2019

NEMC yahamasisha usafi maeneo ya fukwe nchini

 Washiriki mbalimbali wa shughuli ya kufanya usafi katika fukwe ya Andy- Mbezi Beach B jijini Dar es Salaam wakifanya usafi katika eneo la fukwe hiyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma. Zoezi hilo limeratibiwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) kwa kushirikiana na Asasi ya kiraia ya Nipe Fagio, Aspect, Green Waste Pro
na HDIECA.
Kaimu Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) Mhandisi Benjamin Mchwampaka (katikati) akishiriki zoezi la kukusanya taka wakati wa shughuli ya kufanya usafi iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika fukwe ya Andy- Mbezi beach B jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma. Zoezi hilo limeratibiwa na NEMC kwa kushirikiana na Asasi ya kiraia ya Nipe Fagio, Aspect, Green Waste Pro na HDIECA.
 
 
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Baraza la Taifa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikana na Asasi za kiraia zimefanya usafi katika fukwe ya Andy-Mbezi B ikiwa ni sehemu ya maazimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kufanya usafi.

Asasi hizo za kiraia zilizoshirikiana bega kwa bega katika zoezi zima la kusafisha fukwe ni pamoja na Nipe fagio, Aspect, Green Waste Pro. 
 
Akizungumza na Waandishi wa habari wakati wa zoezi la kufanya usafi katika fukwe hiyo Kaimu Meneja wa Kanda ya Mashariki Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhadisi Benjamin Mchwampaka alisema ni muhimu wananchi wakajenga mazoea ya kusafisha fukwe kwani ni eneo linalojumuisha jamii mzima.
 
“Fukwe hii ya Andy imekuwa na uchafu mwingi kutokana na kutofanyiwa usafi kwa muda mrefu hiyo kwa kufanya zoezi hili kutahamasisha wakazi wa maeneo haya kujitoa katika kufanya usafi mara kwa mara ili kufanya mazingira ya fukwe kuwa salama,” alisema Mhandisi Mchwampaka.
 
 Alisema katika zoezi la kufanya usafi wamebaini chupa za plastiki ambazo hazirejerezwi zinazofungashiwa vinywaji mbalimbali ndio zimekidhi katika maeneo mengi ya fukwe na kupelekea mazingira kutokuwa salama kutokana na kukithiri kwa uchafu. 
 
“Tumefanya kuchambua taka katika makundi mbalimbali ili kutupa urahisi wa kubaini aina za taka hususani chupa za rangi na kufatilia mzalishaji ili tusaidiane nae katika kutafuta suluhu la kufanya urejereshaji wa chupa hizo ili kuondoa tatizo hilo,” alisema Mhandisi Mchwampaka.
 
 Alisema tayari kunavijana wamejiajiri kukusanya chupa nyeupe na kujipatia kipato kwa kurudisha kwa mzalishaji kwa ajili ya kuzirejereza hivyo kwa kutumia njia hii iliyoondoa chupa za maji kuzagaa mitaani ndiyo itakayotumika ilikuondoa chupa za rangi. 
 
“Kwa asilimia kubwa taka za plastiki ni janga kutokana na ukweli kwamba kwenye mazingira zinapoingia ardhini zinaweza kukaa muda mrefu bila kuoza na pia kama vinaingia baharini zinakwenda kuharibu ikolojia na kupelekea viumbe wa baharini kupotea,” alisema
Mhandisi Mchwampaka alisema Serikali imepiga hatua kubwa katika kulinda mazingira kwa kukataza matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo ilikuwa ikiendelea kuharibu taswira ya nchi kimazingira na kupelekea maeneo mengi kuhathirika. 
 
“Kauli mbiu kwa sasa katika kuyalinda mazingira ni “Tuungane kuweka mazingira yetu safi na salama Tusibadili vifungashio kuwa vibebeo”, alisema na kuongezea kuwa elimu kwa umma bado inaendelea kutolewakatika kuwajengea uwelewa wananchi juu ya tofauti ya vifungashio na vibebeo.

Aliongezea kuwa tayari Shirika la Viwango Tanzania(TBS) limewataka watengenezaji na waagizaji wa vifungashio na vibebeo vilivyoruhusiwa kisheria wawasiliane na o ili kuwapata maelekezo stahiki juu ya viwango vilivyopitishwa kutengeza na kutumika hapa nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach B, Bi. Fatuma Ramadhan alisema wameshukuru Serikali na wadau wa mazingira kwa kufanya zoezi hilo kwani limezidi kuwapa nguvu wananchi katika kujitoa kwenye shughuli za kijamii kama hivi ambazo manufaa yake ni endelevu. “Changamoto kubwa ya taka kufurika katika fukwe ni kutoaka na maji ya mvua yanayomwaga baharini huja na uchafu mbalimbali hivyo ili kuondoa tatizo hili ni kuhakikisha kila mmoja kaika jamii anawajibika katika kulinda na kusafisha eneo lake ili kupunguza uchafu kuja maeneo ya baharini,” alisema Bi.Ramadhan.

Naye Afisa Mhamasishaji Jamii kutoka Asasi ya Nipe Fagio,Bw.Abdalah Mikulu alisema ushirikiano kati ya wadau wa mazingira wananchi na Serikali kutasaidia kuondoa tatizo la taka nchini na kupelekea mazingira yakawa salama kwa kizazi cha sasa na baadae.
 
 “Tutaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wa mazingira katika kuhakikisha maendeo yote yaliyokithiri kwa takataka tunakwenda kuziondoa na pia kutoa ushauri wa namna bora ya kutunza mazingira nchini,” alisema Bw. Mikulu

No comments:

Post a Comment

Pages