HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 03, 2019

WATAALUMU WA RELI YA SGR KUNOLEWA CHINA

 Na Tatu Mohamed

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimesaini makubaliano na Chuo cha Zhengzhou Railway Vocational and Technical cha China, ili kuwaandaa wataalamu wengi watakaoiendesha Reli ya Kisasa (SGR).

Makubaliano hayo yamesainiwa leo, Juni 3, 2019 katika chuo hicho kilichopo Mabibo, jijini Dar es Salaam na hayo, Mkuu wa NIT, Prof. Zacharia Mganilwa pamoja na Rais wa Chuo cha Zhengzhou Railway Vocational and Technical cha nchini China, Kong Fanshi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya makubaliano hayo, Prof. Zacharia Mganilwa amesema utekelezaji wa mkataba huo utaanza miezi sita ijayo.

Amesema bado nchi inahitaji watalaamu wa masula ya reli, hivyo kuingia kwa makubalinao hayo kutawezesha kuwajengea uwezo wataalamu, kwani walimu wa NIT watakwenda China na wale wa China watakuja NIT, hivyo hivyo kwa wanafunzi wa vyuo hivyo viwili.

"Mbali na hayo pia, tutaweza kuzalisha watunga sera za reli, maafisa usafirishaji wa reli, pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wengine katika sekta ya usafirishaji nchini," amesema na kuongeza kuwa:

"Aidha Walimu kutoka China watakuja nchini kuwafundisha wanafunzi pamoja na wafanyakazi walioko katika mashirika ya Tazara na TRL kuhusu masuala ya uendeshaji wa reli ambapo wataweza kuihudumia SGR yetu kwa ufasaha zaidi," amesema Prof. Mganilwa.

Ameongeza kuwa, China wamekuwa wabobezi wazuri katika masuala ya reli, hivyo ushirikiano huo utainufaisha Tanzania ambayo kwa sasa inakwenda katika uchumi wa viwanda, pamoja na kujenga SGR.

“Unapojenga uchumi wa viwanda ni lazima uwe na reli madhubuti, na ndiyo maana Rais John Magufuli ameamua kujenga reli ya kisasa, sasa tutapata walimu wa kutufundisha kuhusu masuala ya reli na namna gani ya kuiendesha reli yetu tunayoijenga,” amesema Prof. Mganilwa.

Naye Fanshi amesema wamekuja NIT kwa lengo la kuhimarisha ushirikiano na wanaamini mahusiano waliyoyaanzisha yatakuwa na manufaa baina ya vyuo hivyo viwili.

Amesema vyuo vyao vimekuwa vikizalisha wataalamu mbalimbali katika sekta ya usafiri hivyo wataweza kubadilishana uzoefu na kupeana ujuzi katika ufundishaji wa watalam hao.

No comments:

Post a Comment

Pages