WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa mwaka mmoja kwa viongozi wa mikoa
ya Dar-es-salaam, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa, Singida na
Shinyanga ihakikishe iwe imekamilisha kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji.
Pia
amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri zote nchini wahakikishe
wanaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama kile cha Kahama
ili kuharakisha nia ya Serikali katika kuwezesha wananchi kiuchumi.
Ametoa
maagizo hayo leo (Jumamosi, Juni 15, 2019) wakati akifungua Kongamano
la Nne la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi katika ukumbi wa Hazina jijini
Dodoma. Kongamano hilo limeandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi(NEEC) na kauli mbiu yake ni Wezesha Watanzania Kujenga Viwanda.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuliagiza Baraza la Taifa la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuratibu mifuko yote ya uwezeshaji wananchi
kiuchumi ikiwemo ya Serikali na ile ya binafsi ili kujua ipo mingapi na
inamnufaisha nani na je wanufaika wanajijua na ni kweli wananufaika na
kisha wampelekee taarifa.
Waziri
Mkuu amesema mikoa yote iliyokamilisha kuandaa mwongozo wa uwekezaji,
nayo ifikapo mwakani inapaswa kuonesha hatua za utekelezaji katika
kutumia fursa mbalimbali zilizoainishwa pamoja na mikakati ya kutangaza
fursa hizo zilizopo katika maeneo yao.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema matokeo ya tafiti ziliyofanywa na Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuhusu biashara na uwekezaji nchini
yanatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uandaaji wa maandiko ya
miradi mikubwa inayopendekezwa na shirika hilo.
“Miradi
hiyo ni pamoja na ule wa “Harmonized Innovation Solutions for Local
Economic Development” ambao upo katika hatua za maandalizi. Lengo la
UNDP ni kuhakikisha kuwa miradi inayohusu uwezeshaji wananchi kiuchumi
inatekelezwa moja kwa moja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi ambalo lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.”
Amesema
NEEC ina uwezo mkubwa katika kusimamia miradi mbalimbali ya uwezeshaji
ambayo imekuwa ikifadhiliwa na Serikali pamoja na Jumuiya ya Kimataifa
ikiwemo UNDP, ILO, UNCTAD, AfDB na UN-Women, hivyo
ameyahakikishia mashirika hayo kuwa Serikali itasimamia kikamilifu
utekelezaji wa miradi yote ili kupata matokeo yaliyo tarajiwa.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuziagizamamlaka
zote zishirikiane na NEEC kuhakikisha kuwa fursa za uwezeshaji wananchi
kiuchumi zilizobainishwa kupitia tafiti za UNDP zinafanyiwa kazi.
“Aidha, hakikisheni kuwa Miradi mikubwa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi
inatokana na tafiti hizo”
Amesema
anaimani kubwa kuwa kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, malengo
mbalimbali ya nchi kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi yatafikiwa.
Baadhi ya malengo hayo ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
CCM 2015 - 2020; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Dira ya Taifa ya
Miaka 25; na Malengo Endelevu ya Maendeleo ya umoja wa Mataifa (SDGs).
Pia Waziri Mkuu amelitaka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi liendeleekuratibu
masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya
CCM kwa kipindi cha 2015 - 2020 kuhusu uanzishwaji wa viwanda vidogo,
vya kati na vikubwa vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na
misitu.
“Mifuko
ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iboreshwe sambamba na kuongeza ufanisi
ili iweze kuwafikia Watanzania wengi hususan wale wa vijijini. Vilevile,
kamilisheni na hakikisheni mnazindua haraka mfumo wa kupima mifuko ya
uwezeshaji kwa matokeo ya kiuchumi na kijamii na siyo kwa shughuli
walizofanya.”
Amesema
uwezeshaji wananchi kiuchumi ni suala mtambuka, sekta mbalimbali za
kiuchumi na sekta binafsi zinajihusisha moja kwa moja katika kuwawezesha
wananchi kiuchumi, hivyo, amesisitiza kwamba ni muhimu sana masuala ya
uratibu, ufuatiliaji na tathimini ya shughuli za uwezeshaji wananchi
kiuchumi, yakafanywa mara kwa mara ili kuweza kufikia malengo
waliyojiwekea.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma,
JUMAMOSI, JUNI 15, 2019
No comments:
Post a Comment