Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi Kulia, na Mhariri Mkuu wa shirika la
Xinhua Tanzania Si Sibo Li Kushoto, wakisaini mkataba wa Ushirikiano , waliosimama kutoka kulia ni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na
Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe, Katikati ni Bw.He Ping Mhariri Mkuu wa Xinhua
na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha CPC
na Kushoto Wang Ke balozi wa China nchini Tanzania, wakishuhudia tukio hilo.
(Picha na Idara ya Habari MAELEZO).
Kutoka Kushoto Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke, Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe, Mhariri Mkuu wa Xinhua na
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha CPC He Ping, Dkt.Hassan Abbassi Mkurugenzi wa
Idara ya Habari na MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, pamoja na Si Sibo Li
Mhariri Mkuu wa Xinhua Tanzania , wakiwa katika picha ya pamoja baada ya
kusaini makubaliano Jijiji Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu-MAELEZO
Ofisi ya Idara ya Habari MAELEZO
chini ya Wizara ya Habari Utanaduni Sanaa na Michezo, imesaini Mkataba wa
Ushirikiano kati yake na Shirika la Habari la Serikali ya China Xinhua ili
kuimarisha na kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na China ulioasisiwa na Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mao Tse Tung.
Akizungumza katika hafla ya
utiaji saini Mkataba huo iliyofanyika Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe alisema ushirikiano wa
Tanzania na China umekuwepo kwa miaka mingi katika Nyanja mbalimbali na sasa
nchi hizo zimekua kama ndugu.
Waziri Mwakyembe alisema yapo
mambo mengi yalioacha alama kwenye ushirikiano wa kindugu kati ya China na
Tanzania, ikiwemo reli ya Tazara pamoja na uwanja mkubwa wa Taifa Jijini Dar es
Salaam pamoja na majengo mbalimbali makubwa.
“Nafurahi kuona leo wenzetu wa
Idara ya Habari Maelezo wanatiliana saini mkataba wa ushirikiano kati yao na
Xinhua, hii inadhihirisha kukomaa kwa urafiki kati ya Tanzania na China na imeongeza
wigo wa maeneo ambayo nchi hizi mbili zinashirikiana” Alisema Waziri Mwakyembe.
Alisema licha ya kwamba kuna
mashirika ya Habari ya China ambayo yanafanya kazi hapa nchini kama
CCTV,CGTN, XNHUA pamoja na baadhi ya
magazeti, ushirikiano mpya uliosainiwa kati ya Xinhua na Idara ya Habari
Maelezo utaimarisha zaidi sekta ya habari hapa nchini , na pia utasaidia
kubadilishana uzoefu katika masuala ya habari na mawasiliano kwa ujumla.
Kwa upande wake mhariri Mkuu wa
Shirika la Xinhua ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha ukombozi cha
watu wa China CPC Bwana He Ping, alisema amekuja Tanzania kuimarisha uhusiano
wa kindugu ulioasisiwa na waanzilishi wa mataifa haya mawili, na pia kushuhudia
utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Idara ya Habari Maelezo na
shirika la Habari la Xinhua.
Alisema tangu mwaka 1969 Xinhua
imekua ikileta wanahabari wake kufanya kazi hapa nchini, lakini ushirikiano
mahsusi kama ulioanzishwa kati ya Shirika hilo na Idara ya Habari, utasaidia
katika upatikanaji wa habari nyingi za
maendeleo kwani nchi yake inahangaika usiku na mchana kuendelea kuwaletea
wananachi wake maendeleo.
“Lengo letu kama taasisi ya
Serikali ni moja tu kuhakikisha kwamba habari tunazoandika na kusambaza
zinachangia katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kujikita hasa katika habari
za maendeleo, hili linatakiwa kusisitizwa sana kwani katika miaka 40 iliyopita
China ilikua ni nchi inayoendelea lakini kwa sasa imepiga hatua kubwa za
maendeleo duniani” Alisema Bwana Ping.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya
Habari Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi,
alisema habari ni maendeleo na ushirikiano huo ulioanzishwa utaendelea kuleta
chachu ya maendeleo baina ya Tanzania na China hasa katika kipindi hiki ambacho
Tanzania inafanya mageuzi makubwa.
“Sisi tuko tayari kuwapa habari
za kina na zenye takwimu sahihi ili mtusaidie kuieleza dunia kwamba Tanzania
sasa tunapiga hatua, kama mlivyofanya mageuzi makubwa ya kiuchumi huko China na
sisi tunajitahidi kuhakikisha tunakua Taifa lenye maendeleo makubwa na lenye
nguvu kiuchumi” Alisema Dkt Abbasi.
Mkataba uliosainiwa kati ya Idara
ya Habari MAELEZO na Shirika la Xinhua una lengo la kuimarisha uhusiano katika kubadilishana habari na taarifa
mbalimbali, kupitia magazeti na majarida lakini pia kupitia mitandao ya
kijamii.
Aidha katika Ushirikiano huo
Idara ya Habari Maelezo italisaidia shirika la Xinhua katika kupanga na kufanya
mahojiano na viongozi wa serikali, Taasisi na wakala mbalimbali pamoja na
kuwawezesha waandishi wa Shirika hilo kufanya kazi zao kwa wepesi zaidi hapa
nchini.
Katika mkataba huo wa ushirikiano
Idara ya habari pia itawasaidia waandishi wa habari wa Xinhua katika kupata
vibali vya kufanyia kazi hapa nchini pamoja na kuwapatia vitambulisho vya
wanahabari (Press cards).
Kwa upande wa shirikala Xinhua
watasaidia kwenye kutafiti,kuandika na kutoa habari ambazo zinaisaidia Serikali
kupitia Ofisi ya Msenaji Mkuu, pia watahakikisha habari wanazotoa zinz viwango
vinavyokubalika na Idara ya Habari, pamoja na kusaidia ujenzi wa kituo cha
wanahabari (press Center) Jijini Dodoma.
Utiaji saini wa mkataba huo wa
ushirikiano, ulifanywa na Dkt.Hassan Abbasi Mkurugenzi wa Idara ya Habari na
Msemaji Mkuu wa Serikali na Bwana Si Sibo Li ambaye ni mhariri Mkuu wa shirika
la Xinhua hapa nchini.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo
wa ushirikiano, ulihudhuriwa pia na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke,
wawakilishi wa Xinhua kutoka Nairobi Kenya, wawakilishi kutoka Makao Makuu
China, wawakilishi wa Idara ya habari Maelezo, Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo pamona na mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment