Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania
(TFCG), Emmanuel Lyimo akizungumza na madiwani wa Halmashauri ya
Morogoro katika mkutano uliofanyika jana mkoani Morogoro. (Picha zote na Suleiman Msuya).
Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Morogoro, Kibena Kingo akifungua mkutano wa siku moja kwa
madiwani wa halmashauri hiyo uliondaliwa na TFCG, Mjumita na TaTEDO
kujadili namna ya kuendeleza mradi wa Mkaa Endelevu.
Madiwani wa
Halmashauri ya Morogoro wakiwa kwenye mkutano uliondaliwa na TFCG,
Mjumita, TaTEDO kuhusu matokeo ya mradi wa TTCS na namna ya kuendeleza.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
MWENYEKITI
wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kibena Kingo, ameliomba Shirika
la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa
Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la Kuendeleza Nishati
Asili Tanzania (TaTEDO) kuiweka halmashauri hiyo katika awamu ya tatu ya
Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu
'Mkaa Endelevu'.
Kingo
ametoa ombi hilo jana wakati akifungua mkutano wa madiwani wa
halmashauri hiyo uliofanyika mkoani Morogoro kwa kushirikisha madiwani
31 wa kuchaguliwa na 10 wa viti maalum wa wilaya hiyo.
Alisema halmashauri inatambua mchango wa mradi huo kwenye sekta mbalimbali kama elimu, afya, mazingira, maji na miundombinu.
Mwenyekiti huyo aliomba mashirika hayo kuiweka wilaya hiyo kwa mradi wa awamu ya tatu ili waweze kufikia malengo yanayotarajiwa.
"Ni
kweli mmesema Novemba mwaka huu mnamaliza mradi sisi madiwani wa
Halmashauri ya Morogoro tunaomba muingize halmashauri yetu kwenye awamu
ya pili ya mradi tumejipanga kuendeleza," alisema.
Alisema vijiji vitano ambavyo ni vya Mlilingwa, Diguzi, Matuli na Lulongwe vimepata mafanikio ambayo yanapaswa kuendelezwa.
Diwani
huyo wa Ngerengere alisema halmashauri imekubaliana kutumia Msitu wa
Sesenga Lumbachini kutekeleza mradi huo hivyo iwapo mradi wa awamu ya
tatu utahusisha wilaya yao watafanikiwa zaidi.
Kingo alisema TTCS imechochea uhifadhi, uzuiaji uvunaji haramu na holela na utunzaji mazingira hivyo ni mradi wa kuungwa mkono.
Alisema
mradi umesaidia kuondoa wavunaji haramu na kuwa walinzi wa misitu huku
wakijihusisha na miradi ya ujasiriamali kama ufugaji wa kuku na hisa.
Mwenyekiti aliwataka madiwani wenzake kufikisha elimu ya mkaa endelevu kwa wananchi wao ili waweze kuendeleza misitu.
Akizungumza
katika mkutano huo Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema
wameamua kuwakutanisha madiwani hao ili kuwapa hali halisi ya mradi na
waweze kujiandaa kuendeleza wakati mradi unamalizika.
Alisema iwapo madiwani watasimamia na kuendeleza mradi huo vijiji, wananchi na halmashauri watanufaika huku uhifadhi ukiendelea.
Mkurugenzi
huyo msaidizi aliwataka madiwani kutumia Sheria ya Ardhi namba 4 na 5
ya mwaka 1999 kwa vijiji kusimamia ardhi yake kwa kuendeleza kwa miradi
yenye tija.
"Kwa mwaka
zaidi ya hekta 469,000 zinapotea sasa njia ya kukabiliana na hali hiyo
ni vijiji kwa kushirikiana na halmashauri kupitia Sheria namba 4 na 5 ya
mwaka 1999," alisema.
Meneja Mradi wa TTCS, Charles Leonard alisema mradi huo umefanya mapinduzi ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na maendeleo.
Alisema rasilimali misitu ni fursa muhimu kwa vijiji ambavyo vinayo hivyo ni jukumu la viongozi hasa madiwani kuitumia.
No comments:
Post a Comment