SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limeanza kuchukua hatua
kwa wale ambao hawataki kufuata taratibu, kanuni na sheria katika uandaaji na
ushiriki wa mbio mbalimbali za marathon nchini.
Kwa muda mrefu baadhi ya waandaaji wa mbio hizo na washiriki
kutoka nje ya nchi, wamekuwa kwa makusuidi wakivunja taratibu kwa maslahi
binafsi, bila kujali maslahi mapana ya maendeleo ya mchezo wa riadha hapa
nchini.
Mfano wa watu hao ni waandaaji wa Kimondo Marathon iliyofanyika hivi
karibuni mkoani Songwe, ambayo iliendeshwa kinyume cha sheria, taratibu na
kanuni za RT pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Pamoja na jitihada za RT kutuma mjumbe wa Kamati ya Ufundi
(Lwiza John), ili kuwafahamisha waandaaji kwamba wanariadha wa nje ya nchi
hawaruhusiwi kukimbia bila ruhusa ya Vyama vya Riadha vya nchi zao, lakini
mjumbe wetu alipuuzwa na waandaaji pamoja na wanariadha hao watatu waliotoka
nje ya nchi.
Kwa tafsiri rahisi ni kwamba, ubabe ulitumika kwa kisingizio
cha mkuu wa mkoa "kashasema". Je mkuu huyo wa Mkoa ni wa Songwe ama
wa wapi?
Pia tunafahamu kwamba, tuna tatizo kubwa la Mawakala ambao
wanawaleta wanariadha wa nje ili wapate 15% ya fedha wanazoshinda, tutalipeleka
sala hili BMT na kwa Waziri mwenye dhamana ya Michezo.
"Waandaaji wa Marathons wanapaswa kuwa wazalendo kwa
kufuata sheria za RT ambazo pia ni za Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF),
pia wathamini fedha wanazopata kwa wadhamini ambao ni kampuni na taasisi za
kitanzania, zisiende nje ya nchi yetu kiholela sababu hizi ni kodi zetu,".
Kimondo Marathon imeanzishwa kwa nia njema, lakini walikuwa
na masilahi gani na wanariadha wa Kenya ambao hawakuwa na ruhusa?
Wakati RT ikiendelea na hatua zaidi kwa walioshiriki hujuma hizi Kimondo
Marathon, Wanariadha watatu kutoka Kenya,
Denis Kemboi, Limo Peter na Karbolo Tatiyia walioshiriki bila ruhusa,
hawataruhusiwa kushiriki mbio zozote za Tanzania hadi tutakapojadiliana kwa
kina na Shirikisho la Riadha la Kenya (Athletics Kenya).
Tayari tumewaandikia AK na wameonyesha nia njema ya
majadiliano, tunapenda kuwasisitiza waandaaji wote wa Marathons
nchini, kufuata sheria na taratibu na RT itawapa ushirikiano wa kutosha.
No comments:
Post a Comment