Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) Richard
Jordison alipotembelea mgodi huo kufuatilia ulipaji kodi ya pango la ardhi mkoa wa Geita tarehe 10 Julai 2019.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akizungumza katika kikao baina yake na uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita
uliopo mkoani Geita katika ziara yake ya kufuatilia ulipaji kodi ya pango la ardhi
katika taasisi na makampuni mbalimbali yanayodaiwa kodi hiyo tarehe 10 Julai
2019. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Geita Josephat Maganga na
kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) Richard
Jordison. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA
ARDHI).
Na Munir Shemweta, WANNM GEITA
Operesheni maalum
inayofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline
Mabula kupita ofisi moja hadi nyingine kuzibana taasisi na Makampuni yanayodaiwa
kodi ya pango la ardhi imeangukia Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) uliopo
mkoani Geita ambapo imebainika mgodi huo hauna hati miliki ya eneo hilo lenye
ukubwa wa kilomita za mraba 196.27 sawa na takriban hekta 19,927 tangu
kuanzishwa kwake mwaka 2000 na hivyo kushindwa kulipa kodi ya pango la ardhi.
Akiwa katika ziara yake
ya siku moja mkoani Geita tarehe 10, Julai 2019, Dkt Mabula alitembelea Mgodi
huo wa Dhahabu wa Geita kwa lengo la kufuatilia ulipaji kodi ya pango la ardhi
sambamba na kuangalia iwapo mgodi huo una hati miliki ya ardhi katika eneo
hilo.
Hata hivyo, Dkt Mabula
alielezwa na Mshauri wa Masuala ya Sheria ya Mgodi huo Elizaberth Karua kuwa GGML
imekuwa ikilipa kodi mbalimbali serikalini lakini haijawahi kulipa kodi ya pango
la ardhi kwa kuwa ina Leseni Maalum ya Uchimbaji Madini.
Kwa mujibu wa Karua,
Mgodi wa Dhahabu wa Geita ambao uko ndani ya kampuni ya AngloGold Ashanti ya
Afrika Kusini katika kipindi chote cha shughuli zake haujawahi kupewa wito wa
kutakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi na umekuwa ukizingatia Mkataba wa Uendelezaji
Uchimbaji Madini (Mining Development Agreement).
Kwa upande wake Mkuu wa
Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masami
alieleza kuwa, kodi ya pango la ardhi inapaswa kulipwa na haina uhusiano wowote
na leseni za uchimbaji madini kwa kuwa mmiliki wake anakuwa kama amepangishwa
eneo na sheria ya Tanzania imetamka bayana kuwa ardhi itakuwa chini ya Raisi na
kusisitiza kuwa kodi ya pango la ardhi inalipwa kama zinavyolipwa ankara za umeme
na maji.
Kwa mujibu wa Masami, cha
muhimu katika suala la kodi ya pango la ardhi ni umilikishwaji ambapo Mgodi wa
Dhahabu wa Geita unatakiwa kutambulika kwa kuwa na nyaraka sahihi za umiliki na
kusisitiza tafsiri ya sheria ya madini siyo sehemu ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula pamoja na kuipongeza GGML kwa kuwa
mlipaji mzuri wa kodi ya Serikali lakini eneo la Mgodi huo linapaswa kipimwa kutokana
na kuwa katika mipango miji na sheria yake inaelekeza maeneo yote ya mipango
miji kipimwa na kupangiwa matumizi.
‘’Eneo la Mgodi GGML lazima
lipimwe na kupangwa kwa kuwa ndani ya mgodi kuna maeneo ya makazi, ofisi na
matumizi mengine na vyote hivyo lazima vioneshwe katika ramani’’alisema Dkt
Mabula.
Kwa mujibu wa Dkt
Mabula, upimaji katika Mgodi huo wa GGML una faida kubwa kwa kuwa utaondoa
migogoro ya ardhi ambayo baadhi yake husababishwa na wananchi kuingia maeneo ya
mgodi na kutolea mfano Mgodi wa Nyamongo uliopo Tarime mkoa wa Mara baada ya kupimwa
umeepusha migogoro iliyokuwa ikitokea sambamba na kulipa kodi ya pango la ardhi
na kuutaka mgodi wa GGML kueleza ni lini utakuja na majibu wa kutaka kupimwa
eneo lake.
Mshauri wa Masuala ya Sheria
wa GGML Elizaberth Karua aliomba Mgodi huo kupewa muda wa wiki mbili
kushauriana na uongozi wa juu kuhusiana na suala hilo kwa kuwa ujio wa Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ulikuwa wa kushtukiza ambapo Dkt
Mabula aliupa Mgodi huo hadi tarehe 29 Julai 2019 kuja na majibu kuhusiana na suala
hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Mgodi wa Dhahabu wa Geita Richard Jordison alieleza kuwa ofisi yake iko tayari
kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha suala
hilo linafikia muafaka ili kuondoa migogoro.
Taarifa ya idara ya
ardhi katika halmashauri ya Mji wa Geita inaeleza kuwa eneo la mgodi wa GGML
halijapimwa bali lina alama za eneo lenye leseni ya uchimbaji ambazo hazina
rekodi za upimaji na hivyo kuleta ugumu katika kuhakiki maeneo.
No comments:
Post a Comment