Kaimu Mkurugenzi wa Sanaa, Joyce Fisoo, akipiga Zeze kwenye Tamasha la Muziki wa Cigogo, Wilayani Chamwino jijini Dodoma juzi.
Mkurugenzi
wa Kituo cha Chamwino ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tamasha la Muziki wa
Cigogo, Dk. Kedmon Mapana, akilishambulia jukwaa kwenye ufunguzi wa
tamasha hilo.
Na Mwandishi Wetu, Chamwino
SERIKALI imeeleza
kwamba Tamasha la muziki wa Cigogo lililofikia tamati jana kwenye viwanja
Chamwino Ikulu jijini Dodoma ni muendelezo wa heshima ya Tanzania kwa maendeleo
ya sanaa Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza juzi katika
ufunguzi wa Tamasha la 11 la muziki wa Cigogo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sanaa,
Joyce Fisoo alisema heshima nyingine iliyopata Tanzania ni kupata nafasi ya
kuandaa michuano ya Afrika kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON)
sambamba na kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Nchi za Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) unaotarajia kufanyika Septemba mwaka huu.
Fisoo alisema heshima
nyingine iliyoipata Tanzania ni kuwa mwenyeji wa Tamasha kubwa la Afrika
Mashariki la JAMAFEST ambalo ni kichocheo cha ukuzaji sanaa na uchumi wa nchi
wanachama.
Alisema tamasha hilo
la JAMAFEST linatarajia kuanza Septemba 21-28 jijini Dar es Salaam ambako
alitoa wito kwa wadau mbalimbali wa sanaa hapa nchini kuitumia fursa hiyo ya
uwenyeji.
Aidha Fisoo ambaye
alikuwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu Tanzania, alisema kutokana na utendaji
uliotukuka kwa waandaaji wa tamasha la Cigogo, Kituo cha sanaa Chamwino (CAC)
anajipanga kuandaa cheti maalum kwa ajili ya kutambua na kuthamini mchango wa
taasisi hiyo.
“Najipanga kuandaa
cheti mahsusi kwa ajili ya kutambua mchango wa CAC kwa sababu mbali ya sanaa
pia kituo hicho kinatoa elimu kwa mikoa mingine ambayo huhudhuria tamasha hilo
kwa ajili ya kujifunza,” alisema Fisoo.
Fisoo alisema kwa
sababu ya ukubwa wa tamasha hilo, ataishawishi serikali kuliongezea nguvu zaidi
kwa sababu ya maudhui yake.
Mwenyekiti wa tamasha
hilo, Dk. Kedmon Mapana alisema tamasha lake lina wigo mpana wa ufanyaji kazi,
hivyo jamii ya watanzania inatakiwa kuifanyia kazi sanaa.
Dk. Mapana alitumia
fursa hiyo kulitumia tamasha la JAMAFEST kama sehemu ya fursa kwa ajili ya
maendeleo.
Kabla ya tamasha hilo
kuanza, Fisoo na wadau wengine wa sanaa akiwemo Katibu Mtendaji wa Baraza la
Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza, Rais wa Shirikisho la Sanaa za
Ufundi, Adrian Nyangamale na wadau wengineo walitembelea mabanda ya Chuo Kikuu
cha Dar es Salaa (UDSM), Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa),
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Basata, Chama cha
Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Bodi ya Filamu.
Tamasha hilo
lilihudhuriwa na wadau kutoka nchi za Marekani, Uganda, Hispania, Thailand,
Zambia, Ujerumani, Bulgaria, Ethiopia na Argentina.
Kabla ya kuanza kwa
tamasha hilo, mgeni rasmi alikaribishwa na makundi 30 ya ngoma za asili
yaliyoshiriki tamasha hilo.
No comments:
Post a Comment