Wahandisi kutoka Wakala wa
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wakiwa katika ujenzi wa Daraja la Chuma
(Mabey Bridge) lililopo Mto Kihansi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero,
Mkoani Morogoro.
Na Erick
Mwanakulya
Wananchi wa Kata ya Chita Melela
iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro, wameshukuru Serikali
kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) baada ya kutatuliwa
kwa kero yao ya muda mrefu kwa kujengewa Daraja la Chuma (Mabey Bridge)
lililopo Mto Kihansi ambalo linajengwa na TARURA chini ya ufadhili wa Shirika la
Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID).
Hayo yameelezwa na wananchi
waliojitokeza kushuhudia ujenzi wa Daraja hilo linalojengwa na Wahandisi wa Wakala
wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), wakisaidiana na Mhandisi Mshauri Ebenezer
Mollel pamoja na Mtaalamu wa Ufundi John
Hinderer kutoka Kampuni ya Mabey Bridge ya nchini Uingereza.
Wakielezea furaha yao juu ya
ujenzi wa daraja hilo, wananchi hao wamesema kuwa wanaishukuru Serikali ya Awamu
ya Tano kwa kuwajengea daraja maana walikuwa wanapata shida kubwa hapo awali katika
kusafirisha bidhaa zao na kupata huduma mbalimbali za kijamii kwani walikuwa wanatumia
mtumbwi kuvuka Mto ambapo ni umbali takribani Km 1.5.
Kwaupande wake, Diwani wa
Kata ya Chita Melela Mhe. Chelele John amesema, Serikali ya Awamu ya Tano inastahili
kupongezwa kwa maana Daraja hilo ni kiungo muhimu katika uchumi wa Kata yake
pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa maana vyanzo vya mapato katika
Kata za Mlimba, Chita, Mgeta, Mangula pamoja na Mchombe vitakusanywa kwa urahisi
kutokana na uwepo wa daraja hilo.
“Tulikuwa tunatumia mtumbwi
kuvuka Mto na wananchi walipata adha kubwa katika Kijiji chetu kwani kufikia
huduma za kijamii ilikuwa changamoto kubwa, leo hii naona Wahandisi wa TARURA wapo
hapa katika ujenzi wa Daraja hili, hii inadhihirisha kuwa Wakala upo katika
kuhudumia wananchi ipasavyo nasi tunawaunga mkono”, alisema Diwani huyo.
Naye, Mratibu wa TARURA Mkoa
wa Morogoro, Mhandisi Godwin Mpinzile amesema Daraja la Chuma (Mabey Bridge) la
Mto Kihansi limewekwa baada ya kutengeneza barabara ya Chita Melela yenye urefu
wa Km 11.5 na litakuwa mkombozi kwa wananchi wa Chita kutokana na shida wanayoipata
wakati wa mvua na kwamba Wakala utaendelea kuikarabati Barabara hiyo hadi
kuunganisha Kata ya Mlimba ili kuwarahisishia wananchi kufanya shughuli zao za
kila siku.
Pia, amewasihi wakazi wa Chita
kutunza miundombinu ya Barabara pamoja na Daraja kwani gharama kubwa zimetumika
katika ujenzi wa Daraja hilo.
Daraja la kisasa la Chuma (Mabey
Bridge) ambalo limegharimu zaidi ya shilingi milioni 700 ni moja kati ya kazi
za Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika kuboresha Barabara
na kufanya matengenezo pamoja na ujenzi wa Madaraja ili kuwawezesha wananchi
kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Daraja hilo linalenga kutatua
kero ya kudumu kwa wananchi wa Chita Melela kutokana na Madaraja ya hapo awali kusombwa
na maji pale mvua zinaponyesha na linatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment