Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeingia makubaliano na Taasisi ya Udhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), ambapo TTCL imetengeneza mfumo ujulikanao kama 'TTCL HAKIKI' utakaofanya kazi ya kuhakiki mbegu kwa kutumia simu ya mkulima. Mfumo huo utamwezesha mkulima na watumiaji wengine kuthibitisha ubora wa pembejeo za mbegu na vifaa vya kilimo kupitia simu za mkononi na tovuti.
Akizungumza katika hafla hiyo leo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba alisema shirika hilo linatambua umuhimu wa sekta ya kilimo nchini katika kuchania maendeleo kiuchumi hivyo imefarijika kushirikiana na TOSCI kuwasaidia wakulima kubaini pembejeo zisizo na ubora.
"...Sote tunatambua kuwa nchini Tanzania, sekta ya kilimo ni muhimili wa maendeleo ya uchumi. Sekta hii inachangia kiasi cha nusu ya pato la Taifa, robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na chaanzo cha chakula pamoja na utoaji fursa za ajira zaidi ya 75% ya Watanzania,"
"Kwa kutambua ukweli huo na kwa kusukumwa na nia ya dhati ya kutaka kuboresha maisha ya Wananchi wetu, TTCL na TOSCI tunaunganisha nguvu ili kuwapatia wakulima mbegu zilizozingatia viwango vya ubora wa mbegu ambazo ni chanzo kikuu cha mavuno mazuri yatakayompatia mkulima faida zinazoendana na juhudi na uwekezaji wake katika shughulihiyo," alisema Bw. Waziri Kindamba.
Huduma hiyo ya kuhakiki pembejeo kwa kutumia 'TTCL HAKIKI' itakuwa ni bure na kwa simu isiokuwa na mtandao wa internet mkulima atatakiwa kutuma ujumbe mfupi wenye code kwenda namba 15035 zilizopo kwenye kifungashio cha mbegu na mteja wa simu janja atatakiwa kupakua app ya TTCL HAKIKI kutoka play store au kuingia www.ttclhakiki.co.tz .
Katika hafla hiyo ya kuingia makubaliano hayo, Taasisi ya Udhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), iliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Patrick Ngwediagi ambaye alikiri kuwa mfumo huo utawasaidia wakulima na kupunguza mtawanyiko wa mbegu zisizo na ubora.
No comments:
Post a Comment