NA TIGANYA VINCENT
SERIKALI imewataka wazazi kushiriki katika shughuli
za uboreshaji wa elimu na mazingira ya watoto kujifunza ikiwemo ujenzi wa
madarasa ili kupunguza msongamano katika baadhi ya maeneo.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Mwanza na Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) -
anayeshughulikia Elimu Tixon Nzunda wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha
kuandaa vipindi vya redio kupitia Mpango
wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (MKUE-Tanzania).
Alisema kuna baadhi ya wananchi walitafsiri vibaya
tamko la Serikali la elimu bure na kuacha kushiriki katika hata ujenzi wa
madarasa, nyumba za walimu, utoaji wa chakula kwa wanafunzi na kazi nyingine za
kuinua kiwango cha elimu.
Nzunda alisema Serikali iliposema hakuna ada
haikukataza wananchi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo ya elimu kama vile
utoaji wa chakula kwa ajili ya watoto, ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa.
Alisema matokeo ya wananchi kutoshiriki shughuli za
maendeleo ya shule yameanza kujionyesha katika maeneo ambayo wananchi hawashiriki
kwa maendeleo duni ya elimu na kule wananchi wanaposhiriki kumekuwepo na
mafanikio.
Nzuda alisema maendeleo ya elimu nchini yanapaswa
kuwepo na ushirikiano wa utatu yaani Mwalimu, Mzazi na Serikali.
No comments:
Post a Comment