*Asema itakuwa ya bweni ili wasichana
wengi zaidi wasome
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili
kwenye Shule ya Sekondari ya Liuguru wilayani Ruangwa kukagua majengo ya
Shule hiyo na kuzungumza na wananchi, Julai 29, 2019. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua darasa wakati
alipotembelea Shule ya Sekondari ya Liuguru wilayani Ruangwa Julai 29,
2019. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa,
Andrew Chezue. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi kwenye viwanja
vya Shule ya Sekondari ya Liuguru wilayani Ruangwa, Julai 29, 2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
amekuwa na ndoto ya muda mrefu ya kuona shule ya sekondari Liuguru
inabadilishwa na kuwa shule ya bweni kwa ajili ya wasichana pekee.
“Ndoto yangu ni kuona shule hii inakuwa
ya wasichana peke yao. Na tukifanikiwa, tutatengeneza akinamama wasomi,
wanaojitambua, wenye maadili mema na wachapakazi,” alisema.
Alikuwa akizungumza na wakazi wa kijiji
cha Liuguru, kata ya Narungombe, wilayani Ruangwa jana jioni (Jumatatu, Julai 29,
2019) mara baada ya kukagua shule hiyo.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la
Ruangwa, alisema amechagua shule za Mnacho na Liuguru ziwe ni za bweni kwa
ajili ya wanafunzi wa kike tu kama njia ya kuwaongezea fursa za masomo katika
wilaya hiyo.
“Leo nimekuja kuwaeleza ndoto yangu.
Tunahitaji kuona kila mtoto anayeenda shule, anakuwa na uhakika wa kumaliza
masomo yake ya elimu ya juu. Wilaya hii tuna shida ya idadi kubwa ya mimba kwa
watoto wa kike, na mimi hili jambo linanikera sana,” alisema.
“Tulikubaliana tuwe na kaulimbiu yetu
kwamba ‘Ruangwa kwa maendeleo inawezekana’, lakini kwenye elimu tumekwama
kuleta maendeleo kwa sababu dada zetu hawamalizi shule na sisi ndiyo
wasababishaji. Tumeweka sheria ya kuwafunga watu wanaowapa mimba wanafunzi,
lakini bado haisaidii.”
“Njia pekee ya kuondokana na tatizo hili
ni kufanya shule hizi ziwe za bweni ili wakae hapa shuleni, wafundishwe bila
kupoteza muda wa kwenda nyumbani au kukutana na vikwazo wawapo njiani kuja
shule au kurejea nyumbani,” alisema.
“Kwa wenzetu kwenye mikoa mingine, mtoto
wa kike akianza shule ya awali, atamaliza ya msingi, ataenda sekondari hadi
chuo kikuu. Akimaliza kusoma, anarudi nyumbani kuja kufanya kazi kwao na
kuwasaidia wengine waliokosa fursa.”
“Tunahitaji mabweni kwa ajili ya watoto
wetu wa kike kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, tunahitaji nyumba za
walimu ili wake hapa na kuwalea wanafunzi wetu. Yakikamilika, tutawahamisha
wavulana wanaosoma hapa na kuwapeleka shule za jirani au za bweni, ili hapa
tuwaachie wasichana peke yao,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema kwa kuanzia zitatumwa sh. milioni
100 ili zitumike kujenga nyumba nne za walimu, kisha atatafuta fedha nyingine
ajili ya ujenzi wa mabweni, bwalo la chakula, jiko na mahitaji mengine kadri
fedha zitakavyopatikana.
Aliwataka wanafunzi wa shule hiyo
wahakikishe wanakazania masomo kwani hakuna muujiza wa kufaulu mitihani kama
hawatasoma kwa bidii. “Wanangu wa Form 2
na Form 4 hakuna muujiza wa kufaulu
mitihani iliyo mbele yenu. Ni lazima msome kwa bidii. Na msikubali kuishia Form 4, lazima mwende Form 6 na mkimaliza hakikisheni mnafika
chuo kikuu,” alisisitiza.
Mapema, akiwasilisha taarifa
mbele ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Samuel Diwani alisema
shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007, hivi sasa ina walimu 11 ambapo watatu kati
yao wanafundisha masomo ya sayansi na wanane waliobakia wanafundisha masomo ya
lugha na sanaa.
Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 109
ambapo 51 kati yao ni wavulana na 59 ni wasichana, inakabiliwa na changamoto
nyingi zikiwemo ukosefu wa nyumba tisa za walimu, ukosefu wa maabara mbili na
iliyopo moja haijakamilika kwa asilimia 100.
Nyingine ni ukosefu wa mabweni, maabara ya
kompyuta, mfumo wa umemejua, maktaba, jengo la utawala na stoo.
No comments:
Post a Comment