Ofisa
Mkuu wa Wateja Binafsi na Kampuni Ndogo wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi
(wa tatu kulia), akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi
milioni 21 kwa nahodha wa klabu ya gofu ya Lugalo, Japhet Masai,
kwa ajili ya Udhamini wa Mashindano ya Gofu yanayotarajiwa kufanyika
Septemba 7-8 ambapo zaidi ya wachezaji 100 wanatarajiwa kushiriki. (Na
Mpiga Picha Wetu).
Na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI zaidi ya 100 wa Gofu kutoka ndani na nje ya nchi, wanatarajiwa kushiriki mashindano ya wazi kuwania Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF), yanayotarajiwa kurindima kuanzia Septemba 7 mwaka huu yakidhaminiwa na Benki ya NMB.
Mashindano hayo ya kuadhimisha siku ya Majeshi ambayo huadhimishwa Septemba Mosi kila mwaka, hayatafanyika siku hiyo kutokana na ratiba kuingiliana, hivyo kusogezwa mbele hadi Septemba 7.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, nahodha wa timu ya Gofu ya Lugalo, Japhet Masai, alisema mashindano hayo ya wazi ni makubwa, hivyo mcheza Gofu yoyote mwenye uwezo wa kushiriki anakaribishwa kutoka ndani na nje ya nchi.
Alisema mashindano hayo ya wazi hufanyika chini ya Chama cha Gofu Tanzania (TGU), ambapo mwaka huu wanatarajia zaidi ya washiriki 150 kushiriki katika mashindano hayo yaliyopewa nguvu na Benki ya NMB.
“Mashindano haya yanawashirikisha wachezaji wote wa ridhaa na kulipwa, madaraja A, B na C, chini ya miaka 18, pamoja na wakongwe kuanzia miaka 55 na kuendelea,” alisema.
Alisema kwa sasa milango ya kujiandikisha iko wazi na gharama zinafahamika, huku akiwataka wachezaji kuchangamkia fursa hiyo, kwani Septemba 5 dirisha la usajili linafungwa.
Naye Ofisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Wadogo Benki ya NMB, Filbert Mponzi, alisema wao ni benki inayothamini michezo na ndiyo sababu ya kujitosa kudhamini michezo mbalimbali.
Alisema kutokana na mahusiano yao mazuri na Timu ya Jeshi, wamedhamini mashindano hayo kwa Sh. Milioni 21.
“Tumekuwa tukidhamini mashindano haya zaidi ya miaka minne sasa na tutaendelea kudhamini…Hata michuano ya majeshi inayoendelea sasa tumetoa Sh. Milioni 15 kwa ajili ya vifaa, sisi kila sehemu tupo, kwenye soka pia tupo,” alisema.
No comments:
Post a Comment