WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanunuzi wa zao la pamba katika maeneo
mbalimbali nchini wahakikishe wanaongeza kasi ya ununuzi wa zao hilo ili
wakulima waweze kupata fedha zao kwa wakati.
Pia,
Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga pamoja na
Manaibu Waziri wake kubaki katika mikoa yote inayolima zao la pamba hadi
wakulima wote watakapolipwa fedha zao na kuhakikisha pamba yote iliyomo
mikononi mwa wakulima inauzwa.
Ameyasema
hayo leo (Alhamisi, Agosti 8, 2019) wakati alipotembelea Chama cha
Msingi cha Itemelo kilichoko eneo la Dutwa wilayani Bariadi, Simiyu kwa
ajili ya kujionea mauzo ya zao la pamba.
Waziri
Mkuu amesema ataendelea kusimamia mwenendo wa zao hilo kwa ukaribu
lengo likiwa kuona wakulima wananufaika kwa kupata tija. “Ilani ya CCM
ya 2015/2020 inasisitiza kilimo na inataka wakulima wapate masoko ya
uhakika na tunalitekeleza jambo hilo na pamba yote itanunuliwa.”
Amesema
Serikali inataka kuona pamba yote iliyoko kwa wakulima inatoka ili
wakulima waweze kulipwa fedha ambazo zitawawezesha kujikimu kimaisha
pamoja na kununua pembejeo kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka viongozi wa AMCOS wahakikishe wanawatambua
wakulima kwa majina, maeneo wanayoishi pamoja na ukubwa wa mashamba yao
ili waweze kuagiza pembejeo kulingana na mahitaji halisi.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amewasihi wakulima kufungua akaunti katika taasisi
mbalimbali za kifedha lengo likiwa ni kuhifadhi vizuri fedha
wanazozipata kutokana na mauzo ya pamba ili ziweze kuwasaidia baadaye.
Pia,
Waziri Mkuu amewasisitiza wakulima hao waendelee kutunza vizuri pamba
yao na kuipeleka ghalani ikiwa katika hali nzuri ya usafi na ubora wa
hali ya juu, kwani kwa sasa pamba ya Tanzania inasifika kwa ubora katika
soko la dunia.
Kwa
upande wa masoko hususan ya pamba, Waziri Mkuu aliwasisitizia wananchi
wa Dutwa na Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli inaendelea kuhakikisha uwepo wa
masoko ya uhakika wa mazao yote hususan yale ya kimkakati.
Pia,
Waziri Mkuu ameongeza kuwa moja ya agenda muhimu ya ziara yake ya
Kiserikali aliyoifanya nchini Misri mwezi Julai 2019 ilikuwa ni kutafuta
masoko ya uhakika ya mazao ya Tanzania likiwemo na zao la pamba.
Kwa upande wake,
Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally alipokaribishwa kuwasalimu
wananchi alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutoa msukumo katika ununuzi zao la
pamba. Aidha alimuomba Waziri Mkuu aongeze msukumo zaidi ili wakulima
walipwe fedha zao kwa wakati.
Naye,Waziri
wa Kilimo Hasunga amesema kuwa hali ya malipo kwa wakulima wa zao la
pamba kwa sasa ni ya kuridhisha kwa kuwa wakulima katika maeneo
mbalimbali wameanza kulipwa.
Pia
Waziri huyo amemuahidi Waziri Mkuu kwamba wataendelea kubakia katika
mikoa inayolima pamba kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa mauzo ya pamba
ili kuhakikisha wakulima wote wanalipwa fedha zao kwa wakati.
Kuhusu
suala la makato ya fedha za pembejeo ambazo wakulima wanalalamikia
kukatwa kiasi kikubwa kuliko kiwango halisi wanachostahili, Waziri huyo
wa Kilimo amesema atalishughulikia.
Aidha,Mbunge
wa jimbo la Bariadi, Andrew Chenge amesema amefanya ziara katika kata
20 kati ya 30 kwenye jimbo hilo na changamoto kubwa ya wananchi ni mauzo
ya pamba. “Ujio wa Waziri Mkuu umeleta manufaa kwani wanunuzi wameanza
kuja kwa kasi”.
Mbunge
huyo amemuomba Waziri Kuu awafikishie salamu zao kwa Rais Dkt. John
Magufuli kwamba wanamshukuru kwa namna anavyowajali wakulima mbalimbali
nchini wakiwemo na wa zao la pamba.
Kwa upande wake,
Mbunge wa jimbo la Itilima, Njalu Silanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Kampuni ya Nsangali ambayo inanunua pamba amemuahidi Waziri Mkuu kwamba
ifikapo kesho (Ijumaa, Agosti 9, 2019) saa nane mchana atakuwa amelipa
sh. milioni 135 zinazohitajika na amcos ya Itemelo ili kulipia deni la
pamba iliyoko ghalani.
Awali,
Katibu wa Amcos ya Itemelo, Lucas Ephraim alimuomba Waziri Mkuu
awasaidie kuyahimiza makampuni mbalimbali yanayonunua yapeleke fedha kwa
wakati ili kukidhi makisio tarajiwa.
Katibu
huyo alisema chama chao kinahudumia vijiji vitano vikiwa na jumla ya
wakulima 2,665 wa pamba wenye jumla ya ekari 9,675. Pia chama chao
kinahitaji sh. milioni 135.139 ili kulipia deni la pamba ambayo iko
ghalani.
No comments:
Post a Comment