HOSPITALI ya Kanisa la Kilutheri ya Hydom (HLH), ya mkoani
Manyara imeandaa mbio maalumu kwa ajili ya kuchangia miundombinu ya kimatibabu
zitakazofanyika Agosti 10 mwaka huu.
Mbio hizo zenye kauli mbiu ya ‘Run for Life’ zinajulikana kwa
jina la Hydom Marathon na zitafanyika Hydom, Manyara zikishirikisha washiriki
wa makundi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HLH, Dk. Emanuel Nuwass,
kumekuwa na kiwango kikubwa cha vifo hususan vya watoto wachanga katika nchi
zinazoendelea.
Dk. Nuwass, anasema HLH, Mkoa wa Manyara na mikoa ya jirani
nao wanakabiliwa na hali kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ukosefu au
miundombinu mibovu katika kupambana na kupunguza vifo vya watoto wachanga.
“Kutokana na kadhia hiyo, napenda kuwaalika marafiki,
washirika, watu binafsi na taasisi mbalimbali kusaidia katika mpango huo wa
kuokoa maisha ya watoto wachanga kwa kuboresha huduma za miundombinu ya kiafya,
ikiwamo ujenzi wa wodi bora na ununuzi wa vifaa tiba,” alisema Dk. Nuwass.
Hydom Marathon itakuwa na matukio matatu, ambayo ni mbio za
Kilomita 21 ‘Half Marathon’, Kilomita 10 na Kilomita 2 ‘Fun Run’.
Ada ya ushiriki katika Kilomita 21 ni Sh. 20,000, Kilomita 10
Sh. 10,000 na Kilomita 2 Sh. 5,000 ambako kwa wale watu maalumu ‘VIP’ wanaweza
kuchangia Sh. 10,000 kwa kila kilomita moja.
Mkurugenzi huyo mtendaji, aliwaomba washiriki kujisajili
mapema kabla ya tarehe ya mwisho na kwa maelezo zaidi yanapatikana katika
vipeperushi maalumu vinavyopatikana mitandao mbalimbali ya kijamii, ikiwamo ya
HLH na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).
No comments:
Post a Comment