HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 25, 2019

Kampuni ya AGRICOM Africa, Yapongezwa Kwa Zana Bora na za Kisasa za Kilimo

 Mkurugenzi wa Agricom Africa, Angelina Ngalula, akizungumza na waandishi wa habari.


Na Mwandishi Wetu

Serikali imeipongeza Kampuni ya zana za kisasa za kilimo ya Agricom Africa, Tanzania Limited, kufuatia Kampuni hiyo, kuibuka na ushindi wa kwanza kitaifa katika eneo la zana bora na za kisasa za kilimo, uliopatikana katika maonyesho ya Nane Nane kitaifa, yaliyofanyika mkoani Simiyu, kufuatia kampuni hiyo, sio tuu imeleta zana bora za kisasa za kilimo pekee, bali imeleta zana za kisasa za kutengeneza vyakula vya mifugo.


Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Mifugo, Mhe. Luhaga Mpina, alipotembelea kampuni hiyo kujionea zana hizo, baada ya kumalizika kwa maonyesho ya Nane Nane, ambapo Waziri Mpina alisitiza mapinduzi ya kweli ya kilimo, yataletwa na kilimo kinachotumia zana bora na za kisasa, mbegu bora, pembejeo za kilimo na utaalamu wa kisasa wa kilimo, hivyo kubadili kilimo chetu kutoka kilimo cha kujikimu hadi kilimo biashara.


Amesema hata katika sekta ya mifugo, ufike wakati chakula cha mifugo nacho kitayarishwe kama ilivyo kwa vyakula vya binadamu, hivyo kampuni hiyo imeleta vifaa vya kukata majani na kuyafunga kwa ajili ya chakula cha mifugo.


Waziri Mpina ametoa wito kwa halmashauri zote nchini, kununua mashine za kisasa za kilimo na malisho ya mifugo, na kutayarisha mashamba darasa ya kuwafundishia wakulima kwa mifano, ili wakulima wetu waone faida za matumizi ya zana bora na za kisasa za kilimo, na kwa upande wa mifugo, amesema mashine kama hizo, zinaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya wakulima na wafugaji, kwa wafugaji kuandaa malisho ya mifugo yao zaidi ya kuiachia ikizagaa zagaa na hatimaye kula mazao ya wakulima.


Ameitaka kampuni hiyo kusambaza zana hizo kuwafikia wakulima na wafugaji nchi nzima, ikiwa ni pamoja na kuleta vipuri , hivyo amezishauri Halmashauri zote nchini kuwahamashisha wakulima na wafugaji kujiunga katika vikundi ili kuweza kukopesheka, wakopeshwe hizo zana bora na za kisasa ili kuleta mapinduzi ya kweli ya kilimo chetu.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Agricom, Angelina Ngalula, aliahidi kampuni yake kuendelea kushirikiana na serikali katika kuunga mkono juhudi za serikali awamu ya tano chini ya Dr. John Pombe Magufuli, kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kutumia zana bora, na katika kutimiza hilo, tayari kampuni hiyo imeishafungua ofisi katika kanda mbalimbali hapa nchini.


Ili kuwafikia wakulima, kampuni hiyo imeshiriki maonyesho ya nane nane katika kanda tano tofauti, wakianzia Arusha, Mbeya, Dodoma, Morogoro na Nane Nane Kitaifa Nyakabindi, wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, ambapo kampuni hiyo imetwaa zawadi ya kwanza kitaifa katika makampuni ya zana za kisasa za kilimo.


Ngalula amesema Kampuni ya Agricom, ina kauli mbia ya “Toboa Kutokea Shambani”, yenye lengo la kuwahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa za kilimo kwasababu sekta ya kilimo ndio sekta pekee hapa nchini inayoongoza kwa fursa za kuwafanya watu kutoboa na kupata maendeleo ya kweli ya kwao binafsi na pia wakati huo huo kulijenga taifa.


Agricom ni kampuni ya vifaa vya kisasa vya kilimo, yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam, ilianzishwa mwaka 2009 kwa lengo la kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kumiliki zana bora na za kisasa za kilimo, yakiwemo matrekta, combine harvester na zana mbalimbali za kilimo.

No comments:

Post a Comment

Pages