HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 24, 2019

UKILIPISHWA NGUZO ‘NIBIPU’ NITAKUPIGIA – NAIBU WAZIRI NISHATI

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza katika Kongamano la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) lililofanyika Agosti 24, 2019 mkoani Kilimanjaro kumpongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri anazofanya.
 

Na Veronica Simba – Kilimanjaro

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa namba yake ya simu ya mkononi kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na kuwaelekeza ‘wambipu’ ili awapigie na kutatua kero husika, endapo wataambiwa kulipia nguzo, nyaya au mita wakati wakipeleka maombi ya kuunganishiwa umeme maeneo ya vijijini.
Ametoa onyo kali kwa mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ngazi ya Wilaya na Mkoa ambao watakaidi agizo la serikali linaloelekeza kuwa wananchi wote wa vijijini waunganishiwe umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 tu pasipo kulipia kifaa chochote ikiwemo nguzo, nyaya au mita.
Alikuwa akizungumzia yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya nishati, kwenye Kongamano la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mkoa wa Kilimanjaro, leo, Agosti 24, 2019, ambalo lililenga kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazofanya.
“Rais Magufuli alisema tupunguze gharama za kuunganishia wananchi umeme vijijini kutoka shilingi 177,000 hadi 27,000 tu. Atakayekwenda TANESCO akashindwa kuunganishwa kwa bei hiyo au akaambiwa lipia nguzo, lipia waya, lipia mita; Namba yangu ni 0652558010. Nibipu, nitakupigia,” alisema huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Akitoa takwimu za waliounganishiwa umeme vijijini, mkoani Kilimanjaro kwa gharama hiyo ya shilingi 27,000 tangu agizo hilo lilipoanza kutekelezwa mwezi Mei mwaka huu, amesema mpaka sasa idadi imefikia 5,000 huku waliounganishwa kwa mwezi Julai pekee ni zaidi ya watu 2,000.
Amesema Mkoa wa Kilimanjaro unaongoza Tanzania kwa kuwa na umeme katika maeneo mengi ambayo ni asilimia 87.
“Mkoa una Kata 148 ambazo zote zina umeme. Una vijiji 519 ambavyo kati yake, 453 vina umeme. Bado vijiji 66 tu ambavyo vipo wilaya ya Hai (5), Siha (7), Rombo (8), Mwanga (4), Moshi (22) na Same (20).
Amesema, kati ya vijiji 66 vya Mkoa wa Kilimanjaro ambavyo bado havijaunganishiwa umeme, vitabaki 35 kufikia Desemba mwaka huu na kati ya hivyo, serikali imeiagiza TANESCO kuchukua vijiji 18 ili iviunganishe hivyo Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III – 2), utaunganisha vijiji 17 tu vitakavyokuwa vimesalia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, pamoja na mambo mengine, amempongeza Rais Magufuli kwa kuwapa nafasi za uongozi wanawake ambao wameonesha kuwa wanaweza, akitolea mfano wa Makamu wa Rais, Mama Samia Hassan na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu.

No comments:

Post a Comment

Pages