HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 20, 2019

Kanisa latoa miche 5,000 kwa watoto

Paroko wa Kanisa Katoliki Kigango cha Amani, wilayani Muheza mkoani Tanga, Stanslaus Baruti, akionyesha bidhaa wanazozalisha kutokana na mazao ya viungo.

 
NA SULEIMAN MSUYA
 
KANISA Katoliki Kigango cha Amani Kata ya Amani wilayani Muheza mkoani Tanga limetoa zaidi ya miche ya mimea ya viungo ya Karafuu na miti ya asili 5,000 kwa watoto wachanga ili iweze kuwasaidia kuwasomesha.

Hayo yamesemwa na Paroko wa Kanisa hilo, Stanslaus Baruti, wakati alipotembelea Kanisa hilo hivi karibuni.

Paroko Baruti alisema kwa zaidi ya miaka 20 ambayo amekuwepo kijijini hapo amekuwa akiwasaidia wana kijiji kuanzia umri wa mtoto mchanga na wakubwa wanaohitaji.

Alisema wamekuwa wakitoa miche ya miti ya viungo na asili ya kuhifadhi kuwasaidia watoto na wananchi kwa ujumla ambapo lengo la Kanisa ni kuwainua kiuchumi.

“Tumekuwa tukitoa miche 20 kwa watoto wachanga ili wazazi wao waweze kupanda ambapo mtoto akianza darasa la kwanza ameshajiandalia fedha za kulipia masomo yake,” alisema.

Alisema pia anatoa miche ya michungwa kwa wakoma ili waweze kujipatia kipato wakati wa baadae na kuachana na utegemezi.

Baruti alisema miche hiyo wanatoa kwa jamii yote bila kuangalia dini wala kabila jambo ambalo litasaidia kuinua uchumi wa wananchi wa vijiji husika.

Aidha, Paroko Baruti alisema uamuzi wa Kanisa kutoa miche kwa wanakijiji umeungwa mkono na Shirika la Nature Tanzania ambalo liliwapatia shillingi 350,000 ili waoteshe na kugawa.

Pia alisema Nature Tanzania imewapatia nguruwe ambao wanafungwa na Masister wa Kanisa hilo kama mradi wa kiuchumi.

"Kanisa linashirikiana na Nature Tanzania kuhakikisha kuwa jamii ya Amani inabadilika kiuchumi, kijamii na maendeleo kupitia miradi shirikishi," alisema.

Ofisa Program wa Nature Tanzania Nsajigwa Kyonjola alisema shirika hilo limeamua kuwezesha wananchi ambao wanazunguka katika Hifadhi ya Mazingira Asili Amani ambapo kuna viumbe hai vingi na adimu.

Kyonjola alisema shirika hilo linaamini iwapo wananchi watashirikishwa katika uhifadhi kwa kuwezeshwa kiuchumi watakuwa walinzi sahihi wa msitu huo wa aina yake Tanzania.

Kaimu Mkurugeni wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Emmanuel Lyimo alisema wao kama wahifadhi wameamua kushirikia na Nature Tanzania kutoa elimu ya uhifadhi.

Lyimo alisema iwapo wananchi wanaozunguka hifadhi watawezeshwa kwa njia ya kilimo chenye manufaa kwao watakuwa walinzi wakuu wa rasilimali hiyo.

"Hiki kinachofanywa na Kanisa Katoliki Amani ni cha kuigwa na viongozi wote wa dini na wananchi wote wa eneo hili kwani Amani ni Bustani ya Aden Tanzania," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages