MSHIRIKI wa mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC), Musa Dube kutoka nchini Botswana ameishukuru na
kuipongeza Taasisi ya MOI kwa huduma bora baada ya kupata matibabu ya
ugonjwa uliokua unamsumbua.
Dube ametoa keki ya shukrani kwa taasisi ya MOI kama
sehemu ya shukrani na kuridhishwa na huduma bora alizopata. Keki hiyo
ilikua na maneno “Thank you MOI” yenye maana ya ahsante MOI pamoja na
bendera ya Botswana.
Aidha, Dube alikabidhi keki hiyo kwa Mkurugenzi Mtendaji
wa MOI Dk. Respicious Boniface huku jopo la wataalamu waliomhudumia
likishuhudia ambapo alitoa shukrani za dhati kwa huduma bora alizopata.
“Sidhani kama maneno yanaweza kutosheleza shukrani zangu , Ahsanteni sana kwa huduma nzuri, kwakweli nimepata huduma vizuri, ahsante kwa kila aliyeshirkiki kunitibu kuanzia mapokezi, Dk Shabani, Dk Mgisha, Dk Violeth, Elius, Patrick, Josephine na wengine wote, ahsanteni” Alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dk Respicious
Boniface amemueleza Bi Dube kwamba MOI imekua ikitoa huduma kwa wananchi
wa baadhi ya nchi za SADC hivyo kumuomba akawe balozi wa MOI nchini
Botswana.
“Tunakushukuru sana kwa kuamua kurudi kutushukuru kwa
kukuhudumia, tunaimani kubwa kwamba wapo wengine watakuja kutibiwa
Tanzania kwasababu watasikia ulipata huduma bora hapa, wafikishie salamu
waambie tuko tayari kuwahudumia pia” alisema Dk. Boniface.
Taasisi ya MOI imeshiriki katika maonyesho ya wiki ya
viwanda pamoja na mkutano wa 39 wa nchi za SADC ambapo washiriki kutoka
nchi mbalimbali wameshangazwa na huduma bora zinazotolewa na MOI kwa
gharama nafuu ambazo hazipo kwenye nchi zao.
No comments:
Post a Comment