HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 27, 2019

MAANDALIZI MBIO ZA BAISKELI ARUSHA YAPAMBA MOTO

MAANDALIZI mashindano ya  mbio za wazi za baiskeli Arusha yamepamba moto ambapo tayari washiriki kutoka mikoa mbalimbali wamejisajili kushiriki.

Mashindano hayo yanatazamiwa kufanyika septemba 14, mwaka huu ambapo yataanzia maeneo ya Sakina jijini Arusha mpaka Tengeru wilayani Arumeru na kurejea Sakina.

Waandaaji wa mashindano hayo, kampuni ya Rexlex cycling na chama cha waendesha baiskeli mkoani  Arusha wamesema kuwa tayari washiriki kutoka mkoani hapa, Simiyu, Shinyanga, Mwanza na Dar es Salaam wamejitojeza kwa wingi.

Mkurugenzi, kampuni ya Rexlex cycling, Mchungaji, Joel Senny aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa mbio hizo zitawashirikisha waendesha baiskeli waliobobea ambao wataenda kilometa 80, huku wazee wenye umri zaidi ya miaka 45 n a wanawake wakishindana kwenye  kilometa 60 .

"Wengine wataenda kilometa 30, hawa ni wale wanaoendesha baiskeli kwa ajili ya afya zao na kujifurahisha itakuwa siku nzuri sana," alisema Senny na kuongeza

"Tutatumia barabara ya Nairobi Moshi, itakuwa ni njia rahisi kupitika na ina usimamizi wa askari wa usalama barabarani wa kutosha, tutakuwa na magari ya kubeba wagonjwa kiujumla tumejiandaa vizuri," alisema Semmy.

Alisema wote wanaotaka kushiriki ni vema wakalipia tiketi ili waweze kupatiwa namba ya ushiriki vinginevyo itakapotokea mtu anajiunga kwenye mashindano hayo bila namba hiyo ataonekana anafanya vurugu na anaweza kusababisha ajali kwani atakuwa hajapewa maelekezo ya namna ya kushiriki.

Senny alisema zawadi zitatolewa kwa washindi ambapo watakaoshiriki mbio za wabobezi mshindi wa kwanza atapata shilingi, 500,000, mshindi wa pili, shilingi, 300,000 huku mshindi wa tatu akipatiwa shilingi 200,000

Kwa upande wa wanawake na wazee kwenye kila kundi mshindi wa kwanza 150,000, mshindi wa pili, 100,000 na mshindi wa tatu 50,000.

Kauli mbiu ya mashindano hayo ni baiskeli ni ajira baiskeli ni afya kwani kuendesha baiskeli ni mazoezi mazuri kwa afya.

No comments:

Post a Comment

Pages