Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema familia imepata pigo kutokana na
msiba wa kaka yake, Meja Jenerali Alfred Mbowe, aliyefariki dunia juzi.
Meja Jenerali Mstaafu Mbowe
alifariki dunia Julai 28, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
(MNH), jijini Dar es Salaam akisumbuliwa na shinikizo la damu.
Amesema kaka yake huyo, mbali na
kuwa kiungo muhimu katika familia pia alikuwa
msuluhishi wa matatizo mbalimbali
katika jamii.
Akizungumza katika ibada ya kuaga mwili wa marehemu katika Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kunduchi Beach, Mbowe ambaye
pia ni Mbunge wa Hai, alisema familia inamshukuru Mungu kwa kuwapa zawadi ya
Meja Jenerali Alfred (67) ambaye alikuwa kiungo muhimu na kimbilio la familia.
"Tukiwa na changamoto zozote
za kifamilia au za kisiasa tumekuwa tukimwendea na kuomba ushauri wa busara
na amekuwa akitoa ushauri
uliotufanikisha, hivyo ninamuomba Mungu atupatie mtu mwingine angalau wa kushika nafasi
yake" alisema Mbowe.
Akizungumza saa za mwisho alizokaa na
kaka yake, Mbowe alisema : "Julai 27, mwaka huu usiku, familia
iliandaa sherehe ya kumpongeza mdhamini
wa ndoa ya marehemu Alfred kwa kufikisha
miaka 60 ya, ndoa hiyo. Tulisherekea vizuri mpaka saa 7 usiku.
“Nilipotaka kuondoka kaka alinizuia
na kusema "Unaenda wapi sijakaa sana na wewe muda mrefu, hivyo kaa tuongee".
alisema na kuongeza:
"Nikakaa naye na akaniambia
ametoa ahadi ya kuchangia ujenzi wa kanisa
huko Machame, hivyo atajitihada kumaliza kutoa ahadi hizo, lakini cha
kushangaza Julai 28, mwaka huu alifariki dunia," alisema Mbowe.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema kupitia maisha ya kaka yake, aliitaka
familia na jamii kwa ujumla kuwa na uvumilivu na upendo, kwani kifo hicho ni mpango kamili kutoka kwa Mungu.
Pamoja na hayo, alisema jamii kwa kushirikiana na viongozi wanapaswa kuwa na umoja na mshikamano, ili
kuendeleza amani nchini.
Pia Mbowe alitumia fursa hiyo kuwashukuru
viongozi mbalimbali wa serikali, dini na jamii kwa ujumla kwa kutoa msaada wa
hali na mali kufanikisha mazishi ya kaka yake.
Askofu Malasusa
Akiongoza ibada hiyo, Askofu Mkuu
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT ) Dk. Alex Malasusa, aliwataka
waumini wa dini kuishi maisha mema ya kumpendeza Mungu.
Dk. Malasusa alisema jamii inatakiwa
kujifunza kupitia maisha mema aliyoishi marehemu, kwani alikuwa mnyenyekevu,
mwenye kupenda ibada na kujali jamii hadi umauti ulipomkuta.
Alisema marehemu Meja Jenerali
Mbowe hakufa kwa sababu alikosa matibabu bali, Mungu aliamua kumchukua kwa
makusudi yake maalumu.
"Tutumie muda wetu vizuri
tukiwa hapa duniani na kujenga uhusiano
nzuri na Mungu, ili siku akirudi atukute
tuko tayari kumlaki kwenda katika makao yetu ya milele," alisema Dk.
Malasusa.
Pia amewataka waumini kuwa wanyenyekevu,
wenye kupendana na kujali maslahi ya wengine wenye uhitaji, lakini pia
kuimarisha uhusiano na Mungu.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali dini na
vyama vya kisiasa wakiwemo Mawaziri Wastaafu, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa
pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.
Waziri Mwinyi
Awali, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk.Hussein
Mwinyi, aliwaongoza waombolezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Meja Jenerali Mstaafu Mbowe.
Waziri Mwinyi aliongozana na Mkuu
wa Jeshi hilo, Venance Mabeyo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Mbali na Waziri Mwinyi, walikuwapo viongozi wastaafu mbalimbali wa Jeshi hilo ambao
walifika kutoa heshima za mwisho na walipomaliza walienda kumsalimia Mkuu wa
Majeshi Mstaafu David Msuguri anayeugua na kulazwa hospitalini hapo akiwa
amekaa kwenye gari la kutembelea wagonjwa (Wheelchair).
Msemaji wa Familia
Msemaji wa familia, alisema Meja
Jenerali Mbowe aliyekuwa namba ya
uaskari P 2877, alizaliwa Januari 6, Mwaka 1952
na kujiunga na Jeshi la ulinzi la wananchi Tanzania (JWTZ) mwaka 1973 na
kustaafu mwaka 2009.
Alisema mwili wa marehemu
utasafirishwa leo kwenda Machame, Kilimanjaro kwa ajili ya maziko yakayofanyika
Ijumaa. Marehemu ameacha watoto watano, wakiwemo wa kike wawili. CHANZO GAZETI LA TANZANIA DAIMA
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe, akiongoza wanafamilia kuaga mwili wa Meja Jenerali Alfred Mbowe,
ambaye ni kaka yake wakati wa ibada iliyofanyika katika Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kunduchi Mtongani
jijini Dar es Salaam. (Picha na Said Powa).
No comments:
Post a Comment