HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 10, 2019

RC TABORA AZUIA MALIPO YA MILIONI 19/- ZA MKANDARASI

 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akitoa ufafanuzi jana wakati wa Kikao Maalumu cha Baraza la Madiwani ya kupitia hoja ya mbalimbali  kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2017/18.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (mbele) akitoa ufafanuzi jana wakati wa Kikao Maalumu cha Baraza la Madiwani ya kupitia hoja ya mbalimbali  kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2017/18.
Katibu Tawala wa Tabora Msalika Makungu akitoa ufafanuzi leo  wakati wa Kikao Maalumu cha Baraza la Madiwani ya kupitia hoja ya mbalimbali  kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2017/18.


NA TIGANYA VINCENT
 
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imemwagiza Mkurugenzi Uongozi wa  Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kutoilipa Kampuni ya Tingwa kiasi cha milioni 19 ikiwa dhamana baada ya kubainika mapungufu katika ukarabati na upanuzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Mahene.


Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, wakati wa Kikao Maalumu cha Baraza la Madiwani ya kupitia hoja mbalimbali  kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2017/18.



Alisema mradi huo uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 191.5 baada ya ukaguzi umebainika kuwa na kasoro ikiwemo tenki la kuhifadhia maji kuvuja.



Mwanri alisema Kampuni isilipwe fedha zilizobaki hadi atakapofanya marekebisho ambayo hayatasababisha kuvuja kwa maji katika tenki hilo.



“Nawaomba Waheshimiwa Madiwani msikubali kumlipa Mkandarasi huyo fedha zake za ‘retention’ hadi hapo atakapofanya marekebisho ya mapungufu yaliyoibuliwa wakati wa ukaguzi wa CAG hata kama maji yanavuja kidogo dogo ni hasara kubwa inayotokana na upotevu wa maji inaofanyika katika tenki hilo” alisema.



Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameuagiza uongozi kutoa  mpango kazi wa kulipa madeni mbalimbali wanayodaiwa ikiwemo asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani na Mfuko wa Amana.


Alisema  kiasi cha shilingi milioni 185.3 kilitakiwa kukopeshwa kwa  wanawake na vijana lakini fedha hizo hazijakopeshwa kwa wahusika na deni la milioni 765.9 ikiwa linatokana na malipo yasiyostahiki kutoka Mfuko wa Amana.

Mwanri alisema ni lazima kuwepo na mpango unaoonyesha jinsi madeni hayo yatakavyolipwa ili hoja hizo hatimaye zifutwe na CAG.


Wakati huo huo Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu ametoa wito kwa Madiwani na Watendaji kushirikiana katika kuhakikisha wanaharakisha kujibu hoja za CAG kwa wakati.


Alisema kasi ya kujibu hoja za CAG katika Halmashauri nyingi mkoani humo sio nzuri kwani kujibu hoja hizo uko chini ya asilimia 50 na wakati mwingine watendaji wanasubiri wanapokuja Wakaguzi ndio wanaanza kujibu.


Makungu alisema ni vema kila Mtendaji kujibu kwa wakati hoja zinazohusu eneo lake ili kuziondoa na kuhakikisha hazijirudi katika ukaguzi unaofuata.

No comments:

Post a Comment

Pages