Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto), akipeana
mkono na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es salaam- DSE, Moremi
Marwa, alipofanya ziara katika soko hilo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa
bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19, katika taasisi zilizopo chini ya
Wizara ya Fedha na Mipango. (Picha
na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam)
Na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Soko la Hisa la Dar es
Salaam- DSE limetakiwa kuendelea kujiimarisha kwa kutoa elimu kwa wananchi ili
waweze kuwekeza zaidi katika soko hilo lengo likiwa kukuza kipato chao na
uchumi wa nchi.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, alipofanya
ziara katika Soko hilo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti
ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 katika taasisi zilizopo chini ya Wizara
ya Fedha na Mipango.
Dkt. Kazungu
alisema kuwa, idadi ya watu takribani laki tano ambao wamewekeza katika Soko
hilo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watanzania wote ambao ni zaidi ya
milioni 50, hivyo ni vema DSE ikatumia majukwaa mbalimbali kuhamasisha wananchi
kushiriki katika Soko hilo ili kukuza kipato chao kutokana na faida zake.
Alisema
ushiriki wa watu wengi katika Soko hilo hususani walio katika sekta ya uvuvi,
mifugo na kilimo, kutaongeza chachu ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla hasa
katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati uliojikita
katika viwanda.
Kwa
upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Bw. Moremi Marwa, amesema kuwa Soko la DSE lipo kwa ajili ya
kuwezesha wawekezaji kuwekeza katika maeneneo mbalimbali kulingana na bidhaa
zilizopo sokoni.
Alisema ili kuleta bidhaa zaidi katika Soko la
Mitaji, DSE imekuwa ikifanya juhudi kwa kushirikiana na wadau wengine ili
kuziwezesha Serikali za Mitaa na Halmashauri za Miji na Majiji kuweza kupata fedha
kupitia mifumo ya Masoko ya Mitaji ili kuweza kuwekeza katika miradi ya
Maendeleo ya Uchumi na Kijamii.
Alieleza kuwa mifumo ya masoko ya Mitaji katika
Halmashauri inataleta wigo mwingine wa upatikaji wa fedha kwa ajili ya kujenga
miradi ya miundombinu na viwanda katika miji na majiji nchini.
Bw. Marwa alibainisha kuwa
DSE huwapa wajasiriamali, wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na Serikali
kutumia soko kwa ajili ya masuala ya upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na wa
kati katika kusaidia wafanyabiashara kuboresha biashara zao pia kwa Serikali Kuu
kuendesha miradi mbalimbali ya Serikali hasa iliyo katika Bajeti.
“Soko la DSE limekua
kutoka Sh. trilioni 16 hadi trilioni 20 katika kipindi cha miaka minne, hati fungani Sh. trilioni 3.5 hadi trilioni
9.5. na kwa wawekezaji kutoka 220,000 na
sasa 550,000; ukwasi na miamala sokoni imeongezeka kutoka wastani wa takribani Shilingi bilioni 50 kwa mwaka hadi
zaidi Shilingi bilioni 500 kwa mwaka na
katika miamala na ukwasi wa hati fungani kutoka wastani wa Shilingi bilioni 300
hadi kufikia wastani wa takribani Shilingi bilioni 900 kwa mwaka”, alieleza Bw.
Marwa
Bw. Marwa alisema kuwa kumekuwa
na maendeleo mazuri katika vigezo hivyo ambavyo hutumika katika kupima
maendeleo ya Soko, pia DSE imeongeza tija na ufanisi kwa kuwa kampuni
inayojiendesha kwa faida na kulipa faida hiyo kama gawio kwa wanahisa wake,
ikiwemo Serikali.
Alisema kuwa DSE ilipata
uanachama wa kidumu katika Chombo cha Kimataifa kinachosimamia masoko ya Hisa
(World Federation of Exchanges) mwanzoni mwa mwaka huu, ikiwa ni soko la saba
kufikia hatua hiyo barani Afrika.
Afisa
huyo Mtendaji Mkuu wa DSE alisema Soko hilo limewekwa kwenye uangalizi
“Watch-List” na Shirika la Kimataifa la Kupima viwango na ubora vya Uchumi na
Masoko ya Mitaji “Country and Market Classification” kwa nia ya kuifanya DSE
kuwa “Frontier Market Status” ifikapo Septemba Mwaka huu.
Hatua
hiyo inatoa fursa ya kulitangaza zaidi soko kwa wawekezaji wa nje lakini pia
kupata mitaji kutoka kwa wawekezaji wanaotoka nje wanaokuja kuwekeza katika kampuni
na biashara nchini na kwenye miradi mbalimbali.
Soko la DSE limekuwa la
tatu katika masoko 30 yaliyopo barani Afrika kufikia hatua hiyo, masoko mengine
ni Soko la Hisa ni Johannesburg la Afrika Kusini ambalo lina miaka zaidi ya
100, na pia Soko la Hisa la Nairobi (Nairobi Securities Exchange) ambalo lina
miaka takribani 70 tangu uanzishwaji wake, lakini DSE likiwa na miaka 20 tu
na linafanya vizuri katika medani za
kimataifa.
Alisema kuwa DSE ina
bidhaa kuu tatu zilizopo Sokoni ambazo mwananchi yeyote anaweza kuwekeza, bidhaa
hizo ni Hisa, ambapo kuna Kampuni 28 zilizoorodheshwa Sokoni zenye ukubwa wa
thamani ya takribani Shilingi bilioni 19.2. Bidhaa nyingine ni Hati Fungani za
Serikali zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 9.5 na pia Hati fungani za
makampuni binafsi zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 250.
No comments:
Post a Comment