WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania ipo tayari
kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini katika kutimiza azma yake ya
kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo
2025.
Amesema
Tanzania inahitaji uungwaji mkono na Serikali ya Afrika Kusini hususan
katika kipindi hiki ambacho imedhamiria kuimarisha shughuli za
uzalishaji kupitia viwanda kwa lengo la kufikia uchumi wa kati..
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Agosti 16, 2019) wakati wa ziara ya
Kiserikali ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa katika
Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro.
Ameyasema
kwa kuwa changamoto zinazoikabili Tanzania katika nyanja mbalimbali
zinafanana kwa kiasi fulani na zile za Afrika Kusini kwani historia za
nchi hiyo na jiografia vinafana na Serikali ya Tanzania.
Akizungumzia
kuhusu eneo la Mazimbu, Waziri Mkuu amesema kuwa lina uhusiano mkubwa
na historia ya nchi hizo mbili kwa sababu huwezi kuulezea vizuri
uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini pasi na kulitaja eneo hilo.
Waziri
Mkuu amesema eneo la Mazimbu limebeba historia muhimu ya kumbukumbu ya
vuguvugu la ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na mapambano
dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
“Mheshimiwa Rais, Tanzania
ikishirikiana na nchi tano zilizokuwa katika kundi la mstari wa mbele
(Angola, Tanzania, Zambia, Botswana na Msumbiji) ilijishughulisha sana
katika ukombozi kusini mwa Afrika na katika kukomesha sera za ubaguzi wa
rangi nchini Afrika Kusini”.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema kuwa sera za ubaguzi wa rangi zilikoma mwezi
Februari 1994 na kufuatiwa na uchaguzi huru na wa haki uliopelekea
kupatikana kwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo, Hayati Mzee Nelson
Mandela mwezi Mei 1994.
“Tunapoongelea
kukoma kwa sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, siku zote
tutawakumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwal. Julius Nyerere na Hayati Mzee
Nelson Mandela kwa utumishi wao uliotukuka kwa kujenga misingi imara ya
umoja katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini”.
Amesema
misingi imara iliyojengwa na wazee wetu hao, imekuwa chachu ya
ushirikiano kwenye majukwaa ya Kimataifa hususani katika kupambana na
ubaguzi wa kiuchumi na unyanyasaji wa aina mbalimbali.
Waziri
Mkuu amesema namna pekee ya kuwaenzi viongozi wetu hao ni kuendelea
kujenga umoja na kushirikiana katika kuimarisha Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ajili ya maslahi ya wananchi.
Kwa upande wake,
Rais Ramaphosa amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa mchango
mkubwa ulioutoa kwa nchi ya Afrika Kusini wakati wa harakati za
kupigania uhuru wa nchi hiyo, hivyo wataendelea kuimarisha ushirikiano.
Rais
huyo wa Afrika Kusini amesema Serikali yake ipo tayari kushirikiana na
Serikali Tanzania katika kuboresha masuala mbalimbali ya kimaendeleo
ikiwemo kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali na kukuza
teknolojia.
Pia
amesema watairisha chuo cha SUA kwa kuboresha miundombinu mbalimbali
ili kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa. “Tutaboresha na shule katika
eneo hili na kuweka utaratibu wa walimu wake kutembeleana na wa Afrika
Kusini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.”
Rais
Ramaphosa aliwasili katika uwanja wa ndege wa Morogoro saa 4.21 asubuhi
na kupokelewa na Waziri Mkuu. Kisha alitembelea campus ya Solomon
Mahlangu na kujionea maeneo ambayo wapigania uhuru wa Afrika Kusini
walikuwa wakikutana na kupanga mipango mbalimbali.
Pia
kiongozi huyo ambaye kwa mara ya kwanza amefika mkoani Morogoro leo
alitembelea campus ya Mazimbu na kujionea sehemu ambazo waliishi
wapigania uhuru wa nchi yake na kisha aliweka shada la maua kwenye
makaburi ya wapigania uhuru. Ameondoka uwanja wa ndege wa Morogoro na
kuelekea jijini Dar es Salaam saa 1.59 mchana.
No comments:
Post a Comment