HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 09, 2019

TPA, SUMA JKT, 21 Century wajipanga kuteka soko la SADC

Naibu Meneja wa Kiwanda cha Kuzalisha Maji ya Uhuru Peak, Meja Makala Nzinza, akitoa maelezo kwa wajumbe wa Mkutano wa Nne wa Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), waliotembelea kiwanda hicho. Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 5 hadi 8 mwaka huu. (Picha na Suleiman Msuya).
 Wajumbe wa Mkutano na Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC wakiwa katika kiwanda cha Kuzalisha Maji SUMA JKT.


NA SULEIMAN MSUYA
 
MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), imesema ujenzi wa mashine ya kisasa ya kukagua mizigo na gati za kupokea magari vitachochea kukua kwa biashara baina ya Tanzania na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Aidha, Viwanda vya Kuzalisha Maji ya Uhuru Peak cha SUMA JKT na 21 Century vimesema vimejipanga kutumia soko la SADC kuchochea uchumi wa nchi.

Kauli hizo za kutumia soko la SADC kibiashara na kiuchumi zimetolewa na viongozi wa taasisi hizo wakati wakizungumza na wajunbe wa Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC, waliofanya ziara jana kutembelea taasisi hizo jijini Dar es Salaam.

Kaimu Meneja Utekelezaji Kitengo cha  Mizigo Mchanganyiko TPA, Absalom Bohella alisema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani imejikita kuboresha miundombinu ili kurahisisha utoaji mizigo.

Alisema Bandari ya Dar es Salaam inahudumia mizigo ya nchi za Malawi, Zambia, DRC Congo ambazo ni wanachama wa SADC na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kaimu Meneja huyo aliwaambia wajumbe hao kuwa maboresho hayo yanahusu mitambo ya kukagua mizigo na gati ya kushusha magari ambayo itakuwa inaweza kupokea meli yenye uwezo wa kubeba magari 6,000.

"Tangu kufanyika maboresho haya bandari imeendelea kupokea mizigo mingi ya makasha na magari ambapo meli ya mita 300 itaweza kuwaka nanga na kushusha magari 6,000 niziombe nchi za SADC kutumia bandari hii ni bandari salama kama jina lake," alisema.

Alisema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kusomesha vijana wengi kuhusu usimamizi wa bandari halo ambayo imekuwa na tija.

Aisha, alisema ujenzi wa mashine ya kukagua mizigo imepunguza ucheleweshaji wa muda huku ubebaji vitu haramu na vya magendo ukiwa umepungua.

Kwa upande wake Naibu Meneja wa Kiwanda cha Kuzalisha Maji cha SUMA JKT, Meja Makala Nzinza alisema wanajipanga kutumia soko la SADC kuuza maji ya Uhuru Peak ambayo yamepokelewa vizuri na jamii ya Kitanzania.

Meja Nzinza alisema kitendo cha maji hayo kutumika katika Wiki ya Viwanda ni fursa pekee ya wao kujitangaza katika nchi hizo na kwamba wataitumia fursa hiyo kuliteka soko.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha 21 Century, Aminderjit Singh Billu alisema wamekuwa wakisambaza bidhaa zao katika baadhi ya nchi na kwamba mkutano huo umewaongezea nguvu kusambaa katika nchi 16 wanachama.

Billu alisema ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na nchi wanachama umekuwa chachu ya wao kuuza kuendelea kujitanua katika ukanda wa SADC na EAC.

Wakizungumza baada ya ziara hiyo ya kimafunzo Ali Salim Ali, David Msabi na Israel Sosthenes waliwapongeza wadau hao wa maendeleo na kuwataka waondeze juhudi ili waweze kushika soko la SADC kwa ujumla.

Wajumbe hao walisema iwapo sekta zote zitashirikiana kwa pamoja lengo la Serikali kuifanya Tanzania ya viwanda litatimia kwa kasi kubwa.

No comments:

Post a Comment

Pages