Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
akizungumza na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera (hawapo pichani) wakati wa
kikao kazi na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Baadhi ya Watumishi wa Umma mkoani
Kagera wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) wakati wa
kikao kazi chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Prof. Faustin Kamuzora, akitoa ufafanuzi
wa masuala ya kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa kikao
kazi cha Naibu Waziri huyo na Watumishi wa Umma mkoani Kagera chenye lengo la
kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu
wanapowasilisha taarifa za kiutumishi ili kuepuka malalamiko yanahusu stahili
mbalimbali za kiutumishi.
Dkt. Mwanjelwa ametoa maagizo hayo alipokuwa
akizungumza na Watumishi wa Umma mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi
yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuzungumza na
Watumishi wa Umma mkoani humo kuhimiza uwajibikaji.
Dkt. Mwanjelwa amesema zoezi la kusafisha
taarifa za watumishi limeibua kero kwa baadhi ya watumishi kutokana na waajiri kutozingatia
maadili wanapowasilisha taarifa za kiutumishi.
“Awali baadhi ya waajiri waliwasilisha
taarifa za watumishi zisizo sahihi hali iliyosababisha baadhi ya watumishi hao
kupewa stahili ambazo si halali na matokeo yake wakati wa zoezi la kusafisha
taarifa wamekuwa wakibainika kutostahili na hatimaye watumishi hao kuona kama
wameonewa,” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Ameongeza kuwa, mtumishi wa umma anakamilika
kwa kuwa na tabia njema, nidhamu ya kazi, mwenendo mzuri, weledi na ubunifu,
hivyo ni vema kila mtumishi akazingatia hilo ili awe na manufaa kwa umma na
tija kiutendaji.
Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, Serikali
ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha utumishi wa umma unakaa sawa, kama
mtumishi anapaswa kupata haki yake, atapata na kama hastahili aachwe badala ya
kupendelewa,” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Dkt. Mwanjelwa yuko mkoani Kagera
katika ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF na kuhimiza
uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma katika Halmashauri zote za mkoa huo.
No comments:
Post a Comment