Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
ameagiza kuondolewa kwa Bw. Efraz Mkama katika nafasi ya Uratibu wa Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) Mkoa wa Kagera kwa kushindwa kutekeleza majukumu
yake kwa ufanisi.
Dkt. Mwanjelwa ametoa maagizo hayo
kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Prof. Faustin Kamuzora baada ya kutembelea
walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa ya Bukoba kwa lengo
la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kukutana na Watumishi wa Umma
kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri huyo, amesema utekelezaji
wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unapaswa kuendana na kasi ya Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli ambayo ina dhamira ya dhati ya kuziwezesha kaya
maskini kuboresha maisha.
Dkt. Mwanjelwa ameonyesha
kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mratibu huyo wa TASAF Mkoa wa Kagera na hivyo
kutaka nafasi hiyo apewe mtumishi mwingine ambaye ana vigezo na uwezo wa
kutekeleza maagizo ya Serikali kikamilifu kupitia utaratibu wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Dkt.
Mwanjelwa ameridhishwa na mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kutekelezwa kwa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika nyanja za elimu, afya, uzalishaji mali
na ujenzi wa nyumba unaofanywa na walengwa wa mpango huo mkoani Kagera.
“Nimejionea namna wanufaika
wanavyotumia rukuzu wanayoipata kuboresha maisha yao kwa kujenga nyumba bora za
kuishi, kujishughulisha na kilimo, ufugaji na kugharamia mahitaji muhimu ya
elimu na afya,” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Dkt. Mwanjelwa amesema, kwa kutambua
mchango wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Serikali imeamua kutekeleza sehemu
ya pili ya Mpango huo ambayo itatilia mkazo zaidi kwa walengwa kufanya kazi
katika miradi itakayoibuliwa kwenye maeneo yao na kupata ujira kama njia
mojawapo ya kuijiongezea kipato.
Akizungumzia suala la kutotekelezwa
kwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika baadhi ya maeneo, Naibu Waziri huyo
amesema, Serikali imeamua kutekeleza Mpango huo katika maeneo yote nchini ili
kuwafikia wananchi wanaoishi katika mazingira magumu kutokana na umaskini.
Dkt. Mwanjelwa yuko mkoani Kagera
katika ziara ya kikazi kujionea utekelezaji wa shughuli za TASAF na kuhimiza
uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma katika Halmashauri zote za mkoa huo.
No comments:
Post a Comment