WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bw. Shaibu
Ndemanga ampelekee taarifa za utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya Bw. Waryoba Gunza baada ya kushindwa kutoa maelezo kuhusu
utekelezaji wa mradi wa maji kata ya Rutamba.
Ametoa
agizo hilo leo (Ijumaa, Agosti 23, 2019) wakati akizungumza na wananchi
katika Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Rutamba akiwa
katika ziara yake ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo na huduma
za jamii mkoani Lindi.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kumtaka Mkurugenzi huyo atoe maelezo ya
namna gani walivyojipanga katika kutekeleza mradi wa maji kwenye kata
hiyo ambayo wakazi wake wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji na
kushindwa kutoa maelezo.
Kwa
mujibu wa Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Lindi, Bw………alisema mradi wa
kata hiyo unakabiliwa na tatizo la uchakavu wa miundombinu na ukarabati
wake unahitaji bajeti sh. milioni 75 ambazo wameziomba kutoka Wizara ya
Maji.
Waziri
Mkuu amesema miradi yote ambayo gharama zake ziko chini ya sh. milioni
100 inatakiwa itekelezwe kwa kutumia fedha za ndani ya halmashauri
husika. “Miundombinu hiyo ilitakiwa iwe imebadilishwa. Mradi wa sh.
milioni 75 unaomba fedha wizarani ni uvivu.”
Waziri Mkuu amesema suala la huduma ya maji limewekewa msisitizo na Rais
Dkt. John Magufuli kwa kuanzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani,
inayolenga kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama karibu na
makazi yao.
Waziri
Mkuu aliwaambia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati
mizuri inayolenga kuondoa tatizo la maji kote nchini ili kusaidia
wananchi hao hasa wanawake kutumia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo
kuliko kutafuta maji.
Hata,
hivyo Waziri Mkuu amewahakikisha wananchi hao kwamba licha ya kuagiza
mradi huo wa ukarabati wa miundombinu ya kusambazia maji ufanyike kwa
haraka, pia Serikali inatekeleza mradi mwingine wa maji wa Milola ambao
ukikamilika maji yatafikishwa hadi Rutamba.
Wakati huo huo,Waziri
Mkuu amewaagiza Wakuu wa Wilaya nchini wahakikishe wanawasimia vizuri
watumishi wa umma na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kushindwa
kutekeleza majikumu yao ipasavyo.
“Rais
Dkt. John Pombe Magufuli ana nia njema ya kuwapa huduma safi wananchi
wote hadi wanyonge na ameelekeza wahudumiwe vizuri bila ya ubaguzi.
Wananchi kama kuna mtumishi asiyewahudumia vizuri msisite kumtaja kwa
sababu Serikali hii haitomvumia.”
Waziri
Mkuu asema ni lazima kila mtumishi wa umma anayelipwa mshahara kwa
kutumia kodi za wananchi ahakikishe anatekeleza ipasavyo majukumu yake
kwani asipofanya hivyo hatokuwa na nafasi ya kuendelea na kufanya kazi
ndani ya Serikali.
“Watumishi
fanyeni kazi kwa bidii na msitarajie kuundiwa tume pale mnapofanya
vibaya, ukiharibu kazi tunakushughulikia hapo hapo na huu ndio msimamo
wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.”
Waziri
Mkuu amesema kuwa watumishi wanatakiwa wafanye kazi kwa kuzingatia
sheria na kanuni za kazi na pia watambue dhamana kubwa waliyonayo,
ambayo ni kuwahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Amesema
watumshi wa umma hawapaswi kukaa maofisini bali wanatakiwa wapange siku
nne katika juma kwa ajili ya kwenda kutembelea wananchi hususani
waishio maeneo ya vijijini kwa ajili ya kuwasikiliza kero zao na
kuzipatia ufumbuzi.
Waziri
Mkuu amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za jamii ambazo
zilikuwa zikiwakwaza wananchi zikiwemo za miundombinu ya barabara,
tatizo la maji, elimu na afya, lengo likiwa ni kuwawezesha Watanzania
wote waishi vizuri.
Awali,
akizungumza kwaniaba ya wabunge wa mkoa wa Lindi, Mbunge wa Viti
Maalumu, Riziki Lulida alisema wakazi wa kata ya Rutamba wanakabiliwa na
changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji licha ya kuwepo kwa vyanzo,
hivyo aliiomba Serikali iwasaidie.
Hata
hivyo alilalamikia kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira katika
maeneo hayo ikiwemo uvamizi katika vyanzo vya maji pamoja na ukataji
hovyo wa misitu unaohatarisha kuibuka kwa jangwa, ambapo Waziri Mkuu
ameagiza viongozi wa wilaya hiyo kuzishughulikia suala hilo.
No comments:
Post a Comment