HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 13, 2019

Editha: TASAF imeniheshimisha

Mlengwa wa TASAF, Martha Makalla akiwa kazini kwake.


NA MWANDISHI WETU

"MUME wangu alikuwa Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Saruji Tanga. Maisha yetu yalikuwa bora sana tukafanikiwa kujenga nyumba ya vyumba 14 hapa Singida Mjini maeneo ya Majengo.

"Alichanganyikiwa baada ya kufukuzwa kazi akawa mlevi kupindukia, mchafu na mbaya zaidi alikuwa akiniibia hela ndani maana nilikuwa nafanya biashara ndogondogo," anasimilia Editha Makala (53).

Makala ni mkazi wa  Mtaa wa Sokoine Kata ya Misuna, Singida Mjini. Ni mama wa watoto watano na mume aitwaye Braison Makala (63).

Ndoa ya wawili hao ilisongwa na misukosuko kuanzia mwaka 1999 baada ya mume kufukuzwa kazi hali iliyowalazimu kuuza baadhi ya samani zao ili kupata nauli ya kurudi ilipo asili yao, Singida.

Maisha mapya mkoani Singida yalianzia eneo la Majengo kwenye nyumba walioanza kujenga yenye vyumba 14 lakini walipaua vinne ili wapate pa kuishi.

Kwa biashara za kuchoma na kichemsha mahindi, Editha alifanikiwa kuwasomesha watoto wake kwenye shule za serikali hadi vyuo vya elimu ya juu.

"Licha ya maisha magumu sikupenda watoto wangu wakose elimu nilihangaika kwa kukopa, kuomba misaada na biashara ndogo ndogo.

"Ilifika wakati nakosa hela hata ya panadol, kulala njaa haikuwa jambo gumu kwangu na watoto walizoea. Mume mlevi kupindukia hakukubaliana na hali ya kukosa kazi.

"Yeye na pombe ananiibia fedha anaenda kulewa... nilimlilia sana Mungu awavushe watoto wangu kwenye safari ya elimu. Nao hawakuniangusha walikuwa wanafaulu.

"...Dhiki ni kitu kibaya sana maana niliwachikia ndugu na majirani zangu niliowaomba msaada wakaninyima niliwaona wabaya wanafurahia hali yangu," anasema Editha.

Anasema alihama kwenye nyumba yao mwaka 2012 baada ya Benki kuipiga mnada kutokana na kushindwa kulipa mikopo wa Sh. Milioni 2.5 alizokopa ili kufanya matibabu ya bintiye aliyekuwa mwanafunzi wa uuguzi kwenye Chuo cha KCMC mkoani Kilimanjaro.

"Mwanangu wa kwanza Martha, alipata maradhi ya akili akiwa mwaka wa pili kule KCMC nilihangaika sana kumuuguza nikashindwa kuwndelea na biashara nikajiingiza kwenye mkopo benki niliweka ile nyumba kama dhamana.

"Mpaka ilipofikia japo haikuisha ile nyumba thamani yake ilikuwa Sh. Milioni 28 lakini benki waliiuza kwa Sh. Milioni 6.5 tukapewa Sh. 400,000 kwamba ndicho kilichobaki.

"Basi ikabidi ile hela tuifanye sehemu ya kodi na iliyobaki tukaanzia maisha ya vyumba viwili hapa Sokoine mwaka 2012," anasema Editha na kuongeza kwamba hali ilizidi kuwa mbaya huku watoto nao wakiendelea na masomo yao.

Kwa mujibu wa Editha mwaka 2014 alianza kuona afadhali ya maisha baada ya kikao cha wananchi wa Mtaa wa Sokoine kumuingiza kwenye kundi la wakazi maskini zaidi ili awe mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini zaidi (TASAF).

Anasema alianza kupokea Sh. 36,000 aliona miujiza akaweka akiba Sh. 20,000 iliyobaki alinunua dftari za mtoto wake na chakula cha nyumbani.

Anasema aliendelea kushona nguo akiwa na wenzie kazi anayodai kuipenda zaidi huku akifanya biashara ndogondogo nyumbani na stendi.

"Mwanangu Martha anaendelea vizuri ni kwamba amepona yupo tu nyumbani sasa nikawapata kikundi cha wananua nikajiunga nao kushona nguo asubuhi naenda mpaka saa10 jioni naenda stendi kuchoma na kuchemsha mahindi hadi saa6 usiku narudi nyumbani," anasema.

Mlengwa huyo anasema aliendelea kipokea ruzuku ya TASAF hadi akiba yake ilipofika Sh. 100,000 huku akifanya biashara ndipo lilipomjia wazo la kununua cherehani yake ili aendelee kushona akiwa nyumbani.

Anasema baada ya kuingizwa TASAF alijiunga kwenye vikundi vya kuweka na kukopa jambo lililomsaidia kwanza kupata wateja na uhakika wa kukopa hadi Sh. 200,000.

"Kipindi chote nilikuwa napambana ili mume wangu aache kunywa pombe na Mungu alisikia kilio changu nikamshauri tufanye biashara ya maji akakubali. Nikakopa Sh. 200,000 kwenye kikundi nikanunua toroli la kubeba maji na madumu 12 gharama yake ilikuwa 136,000 nikamkabidhi mume wangu akaanza biashara wakati huo nami ile Sh. 100,000 nilinunua cherehani kwa mtu akabaki ananidai Sh.50,000.

"Hiyo ni mwaka jana mwanzoni nikaanza kushona hapa nyumbani napata wateja namshukuru Mungu sasa nami nimekuwa mtu katika jamii TASAF imeniheshimisha sana.

"Mwanangu mdogo Elizabeth yupo shule sasa kidato cha nne nae ananufaika na TASAF kupitia ruzuku ya msichana. Hao wawili ndio nipo nao nyumbani kwa sasa.

"Mwanangu wa pili ni Beatrice huyu alilazimika kuacha shule akaenda kufanya kazi za ndani huko Dar es Salaam mshahara wake alikuwa akitusaidia kwenye mambo mbalimbali mpaka sasa yupo huko mjini.

"Mwanangu wa tatu anaitwa Emmanuel huyu alisoma medical sasa anafanyakazi hospitali ya Mirembe kitengo cha Angaza. Mwingine anaitwa Peter alisoma Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa alipata mkopo wa serikali asilimia 100 akasoma Education sasa hivi yupo jeshini kule Ruvu.

"Ndio wameanza maisha wananisaidia kidogo sio haba ila bila TASAF sijui ningekuwa wapi hivi sasa mume wng anauza maji kwa siku hatukosi Sh. 3,000 na zaidi nami kwenye kushona napatamo... tunao uhakika wa chakula, kulala pazuri na tayari nimenunua kiwanja maeneo ya Nung'una nimelipa Sh. Milioni moja kwa awamu mbili bado Sh. 200,000 nimalizie.

"Sijawahi kukata tamaa na sitafanya hivyo nawashauri wengine pia kufanyakazi kwa bidii hasa biashara ndogondogo wasizidharau zinapesa ila cha muhimu ni kuiheshimu pesa nidhamu ikiwepo tutaachana na umaskini.

"Namshukuru Rais John Magufuli namuomba sana aiongezee nguvu TASAF ili wengi tufaidike nayo mimi  naamini bila huu mpango leo nisingesimama. Kipato cha familia yangu ni Sh. 4,000 kwa siku naweka akiba nia yangu ni kutoka kwenye nyumba ya kupanga ambayo kwa mwezi nalipa Sh. 60,000," anasema Editha.

Mlengwa huyu anasema yupo tayari kuwapisha wengine wenye vigezo kuingia kwenye mpango wa TASAF ili nao wainuke kiuchumi.

Kuhusu TASAF, Braison anasema imemuondoa kwenye aibu ya ufukara na kutengwa na jamii hivi sasa anafurahia maisha.

No comments:

Post a Comment

Pages