Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).
Farida
Ramadhani, WFM, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa ili Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi inahitaji watumishi
takribani 7000 wa kada mbalimbali za kiutumishi.
Hayo yamebainishwa Bungeni Jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb),
wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Tunza Malapo, aliyetaka kujua
ni watumishi wangapi wanahitajika na TRA ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Mamlaka ya
Mapato Tanzania haina upungufu mkubwa kama inavyoelezwa, kwa kuwa idadi ya
watumishi wa TRA walioajiriwa ni 4,751 kati ya 7000 wanaohitajika hivyo kufanya
upungufu kuwa asilimia 28 tu.
Alisema jitihada za kukamilisha idadi
ya watumishi wa Mamlaka hiyo kufikia 7000 zinafanywa kwa hatua, lengo likiwa
kuongeza ufanisi wa kiundendaji na kuendelea kuleta matokeo chanya katika
maendeleo ya nchi.
Alifafanua kuwa tangu Serikali ya Awamu
ya Tano imeingia madarakani imejitahidi kwa kiwango kikubwa kukabiliana na
suala hilo, tayari imeajiri watumishi 692 na katika mwaka wa fedha 2019/20
Mamlaka hiyo imeweka Bajeti ya kuajiri watumishi takribani 150.
No comments:
Post a Comment