HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 11, 2019

HALMASHAURI ZATAKIWA KUHAKIKISHA WATOTO WANAPATA HUDUMA ZA AFYA, ELIMU BILA KIKWAZO

NA MWANDISHI WETU, SINGIDA

MKUU wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Mpango wa Kunusuru Kaya maskini zaidi (TASAF), Zuhura Mdungi, amezishauri halmashauri zote nchini kushirikiana na watendaji wa mpango huo katika kuhakikisha watoto wanapata huduma za afya na elimu bila vikwazo.

Mdungi alisema hayo hivi karibuni wakati maofisa wa TASAF walipotembelea Halmashauri ya Wilayaa ya Singida Vijijiji mkoani Singida, ili kubaini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa mpango huo na kutafuta mbinu sahihi za kukabiliana nazo.

"Mfano hapa wilayani wapo watoto wengi lakini tuliofanikiwa kuwafikia ni 4,092 tunahakikisha wanapelekwa kliniki au hospitali inapobidi na zaidi wanahudhuria masomo yao bila vikwazo naamini uwezo wa TASAF kuwafikia watoto wengi zaidi upo.

"Ilikuwepo changamoto ya watoto kukosa vyeti vya kuzaliwa, haijaisha ndio maana tunaomba ushirikiano zaidi kwa wenzetu wa halmashauri kuhamasisha utoaji na upatikanaji wa vyeti hivyo hasa kwa watoto," alisema Mdungi.

Mdungi pia aliwashauri watendaji wote wanaosimamia walengwa wa TASAF kote nchini, kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa walengwa hao namna ya kuendelea kujiwekea akiba na  kufanya shughuli mbalimbali halali za kujiongezea kipato ili wakifanikiwa waondoke wengine waingie.

"Lengo la mpango ni kuzishika mkono kaya masikini kabisa... tunaamini kwamba wanachopewa si kwa ajili ya kumaliza matatizo yao, ile ni  mbegu ya kuwa-'boost' kutoka pale walipo na kikubwa zaidi kuhakikisha familia inapata milo mitatu na watoto kwenda shule, wanatibiwa inapobidi," alisema Mdungi.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mawasiliano, maofisa wa TASAF wamefanyakazi kubwa ya kuwapatia elimu ya ujasiriamali walengwa ambao sasa kwa kiwango kikubwa wengi wanafahamu namna ya kupangilia pesa zao bila kujali uchache wake na kwamba wapo walengwa waliofanya maendeleo makubwa kiasi cha kuwa mfano wa kuigwa kwenye jamii zao.

"Wapo walengwa wa TASAF waliotengwa kutokana na ufukara wao lakini hivi sasa ni miongoni mwa watu wanaosikilizwa kwenye mikutano ya vijiji kwa kuwa wanatoa mchango wa hali na mali katika maendeleo ya jamii," alisema Mdungi.

No comments:

Post a Comment

Pages