Na Saidina Msangi na Josephine
Majura, WFM, Dodoma
Serikali
imesema kuwa inafanyia kazi ombi la Mbunge
Mbagala la kuifanya Mbagala kuwa Mkoa wa kikodi ili kurahisisha ulipaji wa kodi
ikiwemo ya Majengo.
Hayo
yameelezwa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo , Mhe. Issa Ali Mangungu,
aliyetaka kujua ni lini Serikali
itaifanya Mbagala kuwa Mkoa wa Kikodi ili kuwalahisishia wananchi kulipa kodi.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa, suala la Mbagala
kuwa Mkoa wa Kikodi linafanyiwa kazi ili kuhakikisha shughuli za ukusanyaji wa
kodi zinafanywa kwa ufanisi na kwa urahisi.
Alisema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA ilikusanya
takribani Sh. Bilioni 3.7 katika mkoa wa kikodi wa Temeke katika mwaka wa fedha
2017/2018, ikiwa ni matokeo ya marekebisho
ya sheria ya fedha ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa kufanyika kupitia sheria ya
fedha ya mwaka 2016.
“Mkoa wa kikodi temeke umekusanya kodi kwa asilimia 60
ya lengo la kukusanya takribani Sh. Bilioni 6.1,”alieleza
Dkt. Kijaji.
Kwa
upande mwingine Dkt. Kijaji, amezitaka Benki zote nchini kuwahudumia walemavu wanapofika
kupata huduma za fedha na pia kurekebisha miundombinu ya kuingia ATM ili
kukidhi mahitaji ya walemavu.
Akijibu swali la Msingi la Mbunge
wa Viti maalum Mhe. Amina Saleh
Mollel, kuhusu mpango wa Serikali katika kuhakikisha ATM zinakidhi mahitaji ya
walemavu, Dkt. Kijaji alisema kuwa inaangalia namna ambayo itawezesha mifumo
ya miamala kwa njia ya ATM inakuwa Rafiki kwa makundi yote wakiwemo watu wenye
ulemavu.
“Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu ili
kuhakikisha ATM za mabenki zinawekewa mifumo inayokidhi mahitaji ya watu wenye
ulemavu”, alisema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Mei 2017 Benki Kuu ya
Tanzania ilitoa mwongozo wa mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao ikiwa ni mpango
wa Serikali wa kuhakikisha kuwa huduma za malipo kwa njia ya mtandao zinafanyika
kwa usalama na kukidhi mahitaji ya makundi yote katika jamii.
Aidha pamoja na Serikali kutoa mwongozo huo Benki
nchini hazijafanikiwa kusimika ATM maalum na rafiki kwa watu wenye ulemavu
hususan watu wenye ulemavu wa macho hivyo Benki zinatakiwa kutatua changamoto
hiyo.
No comments:
Post a Comment