Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na ujumbe kutoka nchini Cuba, ukiongozwa na
Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina
Gonzalez, kwenye ukumbi wa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Septemba 9.2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri
wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez
ambapo amewakaribisha Wacuba waje wawekeze kwenye sekta ya kilimo,
hususan cha miwa.
Amekutana
na kiongozi huyo leo (Jumatatu, Septemba 9, 2019) ofisini kwa Waziri
Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. Waziri Mkuu ameishukuruSerikali ya Cuba kwa ushirikiano mzuri inaoutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kuboresha maendeleo ya jamii.
“Tanzania
na Cuba zina uhusiano wa kihistoria. Tunatambua mahusiano mazuri
yaliyopo kati nchi zote mbili, yaliyokuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya
kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere na
Rais wa zamani wa Cuba, hayati Fidel Castro.”
Waziri
Mkuu amesema Serikali ya Cuba imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa
sukari, hivyo amewakaribisha Wacuba waje nchini washirikiane na Serikali ya Tanzania katika kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kuboresha kilimo cha miwa na kuanzisha viwanda vya sukari.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo
kati yake na Serikali ya Cuba kwa kuwa nchi hiyo ni mojawapo kati ya nchi zenye ushirikano wa muda mrefu na Tanzania katika masuala ya kisiasa, kijamii, kiafya na kiuchumi.
”Mfano
katika sekta ya afya, madaktari wengi kutoka Cuba wamekuwa wakija
Tanzania kutibu wagonja waliokuwa na maradhi makubwa na pia Serikali ya
Cuba imekuwa ikitoa fursa kwa Watanzania kwenda kusomea fani ya
udaktari.”
Pia
Waziri Mkuu amewakaribisha Wacuba waje wawekeze katika sekta ya utalii
hususani wa fukwe kwa sababu Tanzania ina fukwe nzuri. Amesema mji mmoja
wa Varadero wa nchini Cuba unaingiza watalii zaidi ya milioni moja kwa
mwaka na unategemea kivutio kikubwa kimoja tu cha fukwe ambayo ina urefu
wa kilomita 22.
Akizungumzia
kuhusu ofisi ya ubalozi wa Tanzania zilizofunguliwa nchini Cuba, Waziri
Mkuu amesema zimesaidia kurahisisha mawasiliano kwa sababu awali
kulikuwa na balozi mmoja tu ambaye alikuwa akiwakilisha nchi ya Cuba
nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez alisema Serikali ya Cuba itahakikisha uhusiano wake na Serikali ya Tanzania unakuwa endelevu. Pia alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.
Kadhalika
kiongozi huyo amesema Serikali ya Cuba imefurahisha na kitendo cha
Serikali ya Tanzania kufungua ofisi ya ubalozi nchini Cuba kwa sababu
imezidi kuimarisha mahusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo
mbili. Kiongozi huyo pia amefanya ziara Zanzibar kabla ya kuja Dodoma.
No comments:
Post a Comment