*Yawataka wadau wajiepusha na vitendo vya rushwa, uvunjifu wa amani
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wadau watakaoshiriki katika uchaguzi wa
Serikali za Mitaa wahakikishe wanajiepusha na vitendo vya rushwa na
uvunjifu wa amani kwani Serikali haitasita kuchukua hatua pale
itakapothibitika vitendo hivyo kufanyika.
Waziri
Mkuu amesema wadau hao mbalimbali kutoka katika Vyama vya Siasa,
Taasisi za Serikali na Zisizo za Serikali na wananchi ni vema
wakahakikisha wanasoma na kuelewa kanuni na miongozo ya uchaguzi huo ili
waweze kushiriki ipasavyo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma. Waziri Mkuu amewataka Watanzania wote wenye sifa washiriki uchaguzi huo kwani ni haki yao ya msingi.
“Natoa
wito kwa Watanzania wote wenye sifa wajiandikishe katika orodha ya
wapiga kura, wachukue fomu za kugombea nafasi mbalimbali na kushiriki
kupiga kura kwani hiyo ni haki yao ya kikatiba kwa kuzingatia misingi ya
demokrasia.”
Mbali
na wadau hao, pia, Waziri Mkuu amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama
vishiriki kikamilifu katika kuhakikisha wananchi wanafanya uchaguzi
kwenye mazingira ya amani na utulivu bila kubugudhiwa.
Waziri
Mkuu amewataka Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi huo
wahakikishe wanazielewa kanuni na miongozo ilitoyotolewa ili waweze
kutoa tafsiri sahihi wakati wa kusimamia uchaguzi huo.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amewahimiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya waratibu vizuri
shughuli za uchaguzi kwenye maeneo yao na wahakikishe uwepo wa ulinzi na
usalama wakati wote wa uchaguzi hasa kipindi cha kampeni na wakati wa
kupiga kura.
Waziri
Mkuu amewasihi wabunge na madiwani wawahamasishe wananchi ili watumie
haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa. “Natoa rai kwenu
mhakikishe mnashiriki kikamilifu katika shughuli zote za uchaguzi huo.”
Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019.
Uchaguzi huo unafanyika kila baada ya miaka mitano kwa lengo la kukidhi
matakwa ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
Mwaka 1977, inayoelekeza kuwa Mamlaka na Madaraka ya Serikali yanatokana
na wananchi.
Kuhusu
uboreshaji wa daftari la wapiga kura, Waziri Mkuu amesema tarehe 18
Julai 2019 Serikali ilizindua zoezi hilo mkoani Kilimanjaro na kuongeza
kuwa uboreshaji huo, unahusisha wapiga kura waliotimiza umri wa miaka 18 na wale watakaotimiza umri huo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.
“Makundi
mengine yatakayohusika ni wapiga kura waliohamia katika kata au jimbo
jingine la uchaguzi, waliopoteza kadi au kuharibika, wanaohitaji
kurekebisha taarifa zao; mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa
yamekosewa pamoja na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa kama vile
kufariki dunia.”
Amesema
kwa sasa zoezi hilo tayari limekamilika katika mikoa ya Kilimanjaro,
Arusha, Manyara, Simiyu, Mara na Mwanza (isipokuwa Halmashauri ya Wilaya
ya Kwimba). Zoezi hilo linaendelea kutekelezwa chini ya kaulimbiu
isemayo Kadi Yako, Kura Yako, Nenda Kajiandikishe.
No comments:
Post a Comment