Mratibu wa Tamasha la Mwalimu Nyerere, Kulwa Karedia, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu kumbukizi ya 20 ya Mwalimu Nyerere inayotarajiwa kufanyika kijijini Butiama mkoani Mara kuanzia Oktoba 8-14. Kushoto ni Mkurugenzi wa Kituo cha Kuhifadhi Utamaduni wa Wazanaki, Mashaka Mgeta. (Na Mpiga Picha Wetu).
NA MWANDISHI WETU
TAMASHA la Pili la Kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere linatarajiwa kufanyika Butiama, Musoma Vijijini mkoani Mara kuanzia
Oktoba 8 hadi 14 mwaka huu likishirikisha matukio ya michezo na kongamano.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Taasisi ya
Kuhifadhi Utamaduni wa Kizanaki, Mashaka Mugeta, tamasha la mwaka huu litakuwa
na kauli mbiu isemayo; “Uadilifu na uchapakazi ni dira kufikia Tanzania ya Viwanda’.
Mugeta,
alisema mwaka huu ukiwa wa 20 Tanzania bila Mwalimu, kwa kushirikiana na wadau
wengine walioko Butiama wameamua kufanikisha tamasha la pili baada ya lile la
mwaka kijijini Butiama.
“Tofauti na matamasha
mengine, tamasha hili linafanyika nyumbani alikozaliwa, kukulia na kuzikwa Baba
wa Taifa. Kama mnavyojua Mwalimu alikuwa na mambo mengi sana katika kulijenga
Taifa hususan uadilifu, upendo, haki, umoja na mshikamano…Na sisi
tunapomkumbuka tunapaswa kuvienzi kivitendo,” alisema Mugeta na kuongeza.
Tamasha la
mwaka huu limegawanyika katika matukio mawili makubwa, michezo na kongamano,
ambako wamewaalika wadau mbalimbali ikiwamo viongozi na mabalozi wa nchi rafiki
zikiwamo Mwalimu alizopigania ukombozi wao.
Alibainisha
kuwa, tamasha hilo halina itikadi na wanapata ushirikiano mzuri kutoka Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ya Butiama na Mbunge wa Musoma Vijijini, hivyo yeyote anayetaka
kushiriki hakuna kipingamizi.
Pia, wameialika
mikoa yote inayopakana na Mara, ambayo ni Kagera, Mwanza, Simiyu na Arusha.
Kwa upande
wake Mratibu wa tamasha hilo, Kulwa Karedia, alisema mwaka huu wameboresha
zaidi kwa kuongeza matukio.
Alisema
mbali na kongamano litazungumzia masuala ya elimu, uhifadhi na mengineyo,
katika michezo wameongeza Netiboli ambayo mwaka jana haikuwepo, Soka, Riadha
Kilomita 10, Kilomita 5 na Kilomita 2.5 kwa watu wazima, Mbio za Baiskeli na
Ngoma za Asili.
Karedia,
aliwahakikishia washindi kuwa zawadi ziko za kutosha na zimeboreshwa.
Mgeni rasmi
katika tamasha la mwaka huu ambalo limeandaliwa na Maranda Investment,
Serengeti Media Centre na Kituo cha Kuhifadhi Utamaduni wa Kizanaki,
anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Jaji Joseph
Warioba.
No comments:
Post a Comment