HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 08, 2019

UMMY: SERIKALI HAINA NIA YA KUZIBANA NGOs

Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bi. Vickness Mayao akitoa taarifa kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu(mbele mwenye kiremba cheusi) kuhusu uhuishaji wa Mashirika yaliyokuwa nje ya Sheria katika zoezi lililofanyika nchini mwezi uliopita katika kikao cha kujadili masuala mbalimbali ya Wizara kilichofanyika jijini Dodoma.  

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali haina nia ya kuyabana Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kutekeleza majukumu yao bali inaweka utaratibu wezeshi wa kuyaratibu Mashirika hayo ili yaweze kuleta tija katika maendeleo ya nchi.
Waziri Ummy ameyasema hayo jana jijini Dodoma wakati alipokutana na watendaji wake kutoka Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii na Idara Kuu ya Afya kwa lengo la kujadiliana na kupata namna bora ya kuboresha huduma ya uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hapa nchini.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Wizara imejipanga kuhakikisha inaweka mazingira bora ya kuratibu Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa ufanisi zaidi ili yaweze kuleta matokeo chanja katika jamii hasa matokeo yanayoonekana na kugusa hali ya maisha ya watu masikini tofauti na kuendesha semina na warsha kama ilivyozoeleka hapo awali.
Amesisitiza kuwa fedha za miradi zinazotumika katika miradi inayotekelzwa na NGOs nchini zitumike kama ilivyopangwana sehemu yenye uhitaji na sio kupeleka miradi sehemu moja na sehemu nyingine kukosa miradi ya maendeleo kutoka kwa wadau wa NGOs.
Waziri Ummy amesema kuwa ni muhimu kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwekeza fedha kwa kufuata vipaumbele vya Taifa ili kuisaidia Serikali katika kuhakikisha jamii inapata maendeleo.
“Kama Wizara tulishataka kufanya maadhimisho mkoa wa Katavi lakini hakukuwa na mdau hata mmoja eneo hilo anayejishughulisha na mradi wa kimaendeleo” alisisitiza Mhe.Ummy
Kwa upande wake Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema kuwa watahakikisha wanaweka mazingira mazuri ya wadau kufanya kazi zao kwani wadau hawa ni kundi muhimu katika maendeleo ya nchi yetu katika kutekeleza majukumu ya kitaifa.
Amesisitiza kuwa kumekuwa na changamoto katika kufanya kazi na wadau wa NGOs hivyo Serikali inatengenza mazingira mazuri ya kutatua changamoto hizo ili kuendelea kufanya kazi na wadau hao katika ulekeo mzuri.
Naye Katibu Mkuu Idara Kuu ya Afya Dkt. Zainabu Chaula amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa Serikali inafuatilia na kujua wadau wa maendeleo wanafanya kazi wapi imeamua kuja na mfumo wa Wadau Portal utakaosaidia kuonesha wadau walipo nchini na wanatekeleza miradi ipi na wapi.
Ameongeza kuwa dhamira ya juhudi zinazofanywa na Wizara ni kuhakikisha kuwa panakuwepo miongozo na mifumo ya utoaji huduma kwa wadau itakayosaidia kuratibu, kusimamia na na kubaini kwamba ni kwa kiasi gani wadau wa maendeleo wanachangia katika juhudi za Serikali za kukuza maendeleo na ustawi wa maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Pages