KITUO cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) kimetoa wito kwa serikali kufuta adhabu ya kifo nchini
katika sheria zinazoainisha kosa hilo na kuweka adhabu mbadala.
Wito
huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Kituo hicho, Naemy Sillayo wakati wa maadhimisho ya 17 siku ya kupinga
adhabu ya kifo, ambapo pia walizindua makala fupi ya video inayohusu
wazee walioachiwa baada ya kuhukumiwa kunyongwa.
Alisema
LHRC ni mwanachama wa mtandao wa kupinga adhabu ya kifo duniani ‘’World
Coalition Against Death Penalty’’ na wanaendelea kuelimisha umma juu
ya madhara yanayoweza kutokana na adhabu hiyo sambamba na kuhamasisha
serikali kubadilisha adhabu hiyo kuwa adhabu ya kifungo cha Maisha.
Alibainisha
kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania, 2018 jumla ya
watu 480 wapo kwenye orodha ya watu waliohukumiwa adhabu ya kifo wakiwa
gerezani kusubiri kunyongwa.
Aliongeza
kuwa, Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977
inalinda haki ya kuishi kwa kila mtu. Hata hivyo, ibara hii inaathiriwa
na Sura ya 16 ya Sheria za Makosa ya Jinai zinazoweka adhabu ya kifo kwa
kosa la uhaini, mauaji na ugaidi.
"Pamoja
na mtazamo chanya ya Rais John Magufuli ikiwemo kauli aliyoitoa mwaka
2017 akiwa anamuapisha Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma
akieleza nia yake ya dhati ya kutokutia saini adhabu hiyo kwa ajili ya
utekelezaji pamoja na kuwasamehe wafungwa 61 waliohukuwiwa kunyongwa
katika sherehe za uhuru mwaka 2017, bado LHRC inasisitiza uwepo wa
utayari wa kufutwa kwa adhabu hiyo katika sheria na kuwa na adhabu ya
kifungo cha maisha kama adhabu mbadala.
"Lengo
la wito huu si kuwatetea wahalifu bali ni kupunguza madhara ya adhabu
hii ya kikatili kwa jamii na kuendelea kulinda haki ya kuishi. Tunaiomba
ibadilishe iweke adhabu nyingine isiyohusisha kuua au kifungo cha
maisha," alisema.
Alitaja
baadhi ya sababu za kupinga adhabu hiyo, kuwa ni ya kikatili na
inakiuka haki ya msingi ya kuishi na kudumisha utamaduni wa ‘jicho kwa
jicho' pia inapingana na misingi ya haki za binadamu kwa vile ni adhabu
ya kikatili inayokatisha haki ya binadamu ya kuishi.
Pia
alisema adhabu hiyo ikishatekelezwa haiwezi kubadilishwa, hata kama
kuna makosa yametokea na Nchi nyingi duniani zimeendelea kuondoa adhabu
ya kifo na kuacha kutekeleza adhabu hiyo.
"Mnamo
Oktoba 2, mwaka huu 2019, nchi ya Angola imeridhia mkataba wa nyongeza
wa hiari kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za kisiasa na kiraia wa
1966 na kufuta adhabu ya kifo katika nchi zao na hivyo kufanya idadi ya
nchi zilizoridhia mkataba huo kufikia 88.
"
Sababu nyingine ni kwamba waathirika wengi wa adhabu hii ni watu
maskini ambao hawana uwezo wa kupata mawakili wabobevu kuwawakilisha
katika kesi zao. Pia ni vigumu kuhakikisha kuwa inatekelezwa tu kwa wale
watu ambao wametenda na kukutwa na hatia ya kosa hili au wabaya zaidi
na adhabu hii haimpi nafasi mtuhumiwa kujirekebisha bali ni ya kulipiza
kisasi," alisema.
No comments:
Post a Comment