HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 10, 2019

Makumbusho ya Nyerere kuwa kitega uchumi Tabora Boys

 Baadhi ya nukuu za Mwalimu Nyerere zikiwa kwenye kuta mbalimbali za shule ya Tabora wavulana alizoziandika enzi za uhai wake.
 Wanahabari wa kike na maofisa habari wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakiwa kwenye chumba maalum kilichohifadhi historia ya Mwalimu Nyerere katika shule ya Tabora wavulana.
 Muonekano wa chumba chenye historia ya Mwalimu zikiwemo nukuu na machapisho mbalimbali aliyoyaandika enzi za uhai wake.
Baadhi ya wanafunzi na maofisa wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakiwa kwenye picha ya pamoja mbele ya mlango wa kuingia kwenye jengo la utawala la shule ya Tabora Wavulana.

Na Irene Mark, Tabora

MKUU wa shule ya Sekondary Tabora Wavulana, Deograsias Mwambuzi amesema wanatarajia kutumia historia ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa kitega uchumi cha shule hiyo.

Akizungumza na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali waliotembelea shule hiyo aliyosoma hayati baba wa taifa alisema wameona fursa hiyo kutokana idadi kubwa ya wageni wanaotembelea shule hiyo kujifunza historia ya Mwalimu Nyerere.

Wanahabari hao na baadhi ya maofisa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, wapo kwenye ziara ya kutembelea shule alizosoma na kufundisha hayati baba wa taifa, Mwalimu Nyerere wakati taifa likiadhimisha miaka 20 baada ya kifo chake na kuhakikisha historia yake kwenye elimu inahifadhiwa vema.

Alisema taratibu za kuifanya makumbusho hiyo ya baba wa taifa kuwa sehemu ya kitega uchumi zimeanza kwa kumshirikisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Mkuu huyo wa shule alisema baada ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kufanya makumbusho makubwa katika shule hiyo yameongeza hamasa ya wageni kutembelea shule hiyo na kujifunza historia ya kinara wa harakati za ukombozi wa Tanganyika na Tanzania.

"Naishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi ma Teknolojia wametusidia kuboresha vyumba 17 vya madarasa, Ofisi 10 za walimu, vyoo 15 na maktaba moja mpya.

"...Maboresho hayo pia yalihusisha mfumo wote wa umeme na uondoaji wa maji ya mvua ndio maana leo unaona mazingira ya shule yetu ni mazuri," alisema Mwalimu Mwambuzi.

Alisema shule ya Tabora iliwekwa jiwe la msingi mwaka 1922 na kuanza kazi mwaka 1925 hivyo ni shule yenye historia kubwa kwa nchi kwa kuwa viongozi wengi waliopambania uhuru walisoma hapo.

"Wakuu wa mihimili mitatu ya dola wamesoma hapa, Waziri Mkuu na baadae Rais wa kwanza wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere ametoka hapa, Spika wa kwanza wa Bunge, Adam Sapi Mkwawa alikuwa hapa na hata Jaji Mkuu wa kwanza pia alisoma Tabora school.

"...Mawaziri, wabunge na majaji wengi walisoma hapa kwa hiyo shule hii ni kisima na chimbuko la viongozi wa taifa hili na bado tunaendelea kupika viongozi hapa," alisema Mwalimu Mwambuzi.

Kwa mujibu wa historia ya shule ya Tabora, watoto wa watalala wa Uingereza na machifu wa Tanganyika ndio pekee waliosoma shule hiyo.

"Watoto wa wakoloni na machifu hii ndio ilikuwa shule yao na iliitwa Tabora school licha ya kuwa na upande wa wavulana na wasichana. Baada ya Serikali kuichukua kutoka kwa wakoloni ilipofika mwaka 1990 ikaitwa Tabora wavulana na ile nyingine ikaitwa Tabora wasichana," alisisitiza mkuu huyo wa shule ya Tabora wavulana.

No comments:

Post a Comment

Pages