Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo
Pinda, wakati alipowasili kufungua Mkutano wa Wadau wa Lishe jijini
Dodoma. Katikati ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema utapiamlo
ni miongoni mwa vikwazo vya kutimiza dhamira ya Serikali ya awamu ya
tano ya kujenga uchumi wa viwanda ambao utawezesha Taifa kufikia uchumi
wa kati ifikapo mwaka 2025.
Amesema
bila ya kuwa na lishe bora na afya njema, vinavyosaidia kuongeza uwezo
wa kuelewa na ubunifu ili kuhimili ushindani wa kiuchumi nchi haitafika
kwa wakati kwenye uchumi wa kati na wa viwanda uliokusudiwa.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 3, 2019) wakati akifungua
mkutano wa mwaka wa Wadau wa Lishe uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina
jijini Dodoma. Amesema ni muhimu elimu ya lishe ikatolewa kwa wananchi
wote.
“Pamoja
na tafiti kuonesha kwamba tumepunguza viwango vya udumavu na upungufu
wa damu bado viwango vyake havikubaliki kimataifa. Vilevile, tuna
viwango vya utapiamlo ambavyo vimezidi kuongezeka na havikubaliki
kimataifa ikiwemo uzito uliozidi kwa wanawake wenye umri wa kuzaa.”
Amesema
hali hiyo ni hatari kwa nchi ambayo inayokabiliwa na aina nyingine za
utapiamlo unaosababishwa na lishe duni kama udumavu, utapiamlo mkali na
wa kadiri ambapo athari zake ni kubwa katika ukuaji wa watoto wenye umri
wa chini ya miaka mitano. “Hii ni ishara tosha kwamba tunatakiwa
kuongeza juhudi katika kupambana na aina zote za utapiamlo ili kufikia
viwango vinavyokubalika Kimataifa.”
Amesema
Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutoa kipaumbele kwa
maeneo ambayo yameathirika zaidi na ambayo yanatekeleza miradi
inayolenga kupunguza udumavu kwa watoto, matatizo ya upungufu wa vitamin
na madini.
Kipaumbele
kitatolewa katika kuimarisha matibabu ya utapiamlo mkali na wa kadiri,
kupunguza tatizo la uzito uliokithiri na viriba tumbo na tatizo la
upungufu wa damu kwa wanawake na watoto ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo
inaleta matokeo chanya katika maeneo hayo.
Amesema
kuwa mipango yoyote wanayojiwekea haiwezi kuleta matokeo chanya bila
kuitengenezea mikakati thabiti ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na kutenga
rasilimali za kutosha, ambapo wataalamu hao waibue mikakati itakayoweza
kutumika katika kupunguza tatizo la utapiamlo.
Pia,
Waziri Mkuu amewataka waajiri wote waandae fursa na kuwaalika mahala pa
kazi maafisa lishe ili kuongeza ufahamu wa watumishi kuhusu lishe bora.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais-TAMISEMI
zimetakiwa ziweke mipango ya kuhakikisha maafisa lishe wanaalikwa kutoa
elimu sambamba na ufundishaji shuleni.
Kwa upande wake,Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye
Ulemavu Jenista Mhagama amesema bila kuwa na nguvu kazi yenye lishe na
afya bora Taifa haliwezi kufanikiwa kwenye masuala ya elimu, kilimo,
viwanda hivyo kukwamisha jitihada za Serikali ya awamu ya tano ya
kujenga uchumi wa viwanda.
“Kwa
hali iliyopo sasa ni wazi kuwa bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili
kuondokana na utapiamlo nchini. Juhudi za pamoja zinahitajika ili kuweza
kufikia malengo tuliyojiwekea katika Mpango Jumuishi wa Taifa wa Lishe
(2016/17 – 2020/21), ambayo ni pamoja na kupunguza udumavu kwa watoto
wenye umri chini ya miaka mitano kufikia asilimia 28 na uzito uliozidi
kufikia asilimia 30.”
Amesema
Serikali inatambua kuwa lishe ni suala mtambuka linalotegemea jitihada
za sekta mbalimbali, ambapo waliandaa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa
miaka mitano kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2020/21 ili kutoa muongozo
katika utekelezaji wa afua mbalimbali za masuala ya lishe.
Naye,
Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema katika jitihada za kupambana
na umasikini ni vema elimu ya lishe bora ikatolewa kwa wananchi wote,
ambapo amemshauri Waziri Mkuu aibebe agenda ya lishe, ambapo Waziri Mkuu
amekubali.
Waziri
Mkuu huyo Mstaafu ameongeza kuwa, mila potofu nazo zimechangia suala la
utapiamlo nchini kwa sababu katika familia nyingi nchini vyakula vingi
vizuri wanapewa wanaume na vyakula vibovu wanakula wanawake na Watoto.
Awali,
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt.
Faustine Ndungulile amesema udumavu umepungua kutoka asilimia 34.4
mwaka 2015 na kufikia asilimia 31.5 mwaka huu.
Dkt.
Ndungulile alisema licha kupungua kwa udumavu, changamoto iliyopo kwa
sasa ni suala la unyonyeshaji kwa watoto walio na umri wa chini ya miezi
sita, wanaonyenyeshwa ni asilimia 58 tu, huku asilimia 30 ya Watoto
wenye umri wa zaidi ya miezi sita hawalishwi vizuri.”Theruthi moja ya
wanawake nchini wana viribatumbo na utapiamlo wa lishe iliyopitiliza.
No comments:
Post a Comment