Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
(katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Sumbawanga pamoja na viongozi wengine.
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo, amewapongeza
madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kwa kuweza kutekeleza
agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa tarehe 6, Oktoba 2019 alipokuwa
katika ziara yake ya siku 3 ambapo aliiagiza halmashauri hiyo kuhamia Laela
pamoja na halmashauri nyingine nchini kuhamia katika maeneo yao ya kiutawala.
Amesema kuwa ni watumishi 16 tu kati ya watumishi 165
wa makao makuu ya halmashauri wanaotumia mifumo ya watumishi (LAWSON), mfumo wa
mapato LGRCIS), Mfumo wa malipo wa EPICOR, TASAF na Kitengo cha Uchaguzi ndio
waliobaki mjini wakisubiri miundombinu hiyo kukamilika katika makao mapya ya
halmashauri hiyo katika Mamlaka ya mji mdogo wa Laela.
“Nitoe maelekezo kwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kushirikiana na Wadau wengine
(Mfano TTCL) ahakikishe anaunganisha Makao Makuu Mapya ya Halmashauri Laela
kwenye Mkongo wa Taifa. Hii itawezesha
Mifumo mingine inayotumia Mtandao wa mawasiliano kuweza kufanya kazi kutokea
hapa hapa Laela. Ninamuagiza Mkurugenzi
wa Halmashauri kuhakikisha Watumishi ambao bado hawajahamia Laela wawe
wamehamia ifikapo tarehe 1 Januari, 2020.” Alisema.
Aidha, ameitaka
menejimenti ya halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wadau kufanya tathmini juu ya
kuwafikia wananchi waliopo mbali na Laela kama vile kutoka katika vijiji vya
mfinga, Mwadui, Kalumbaleza wanaokwenda kupata huduma Laela ambao wanatoka
umbali wa zaidi ya kilometa 150.
Ameyasema hayo katika
kikao cha baraza la madiwani la kwanza kufanyika katika makao makuu hayo mapya
ya halmashauri hiyo tarehe 21.11.2019, kikao kilichohudhuriwa na viongozi wa
vyama mbalimbali vya siasa, madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri.
Awali akitoa taarifa ya
maandalizi ya kuhamia katika makao hayo mapya Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt.
Khalfan Haule alisema kuwa kitengo cha uchaguzi kimebaki mjini kutokana na
kukosekana kwa eneo kubwa la kuhifadhia vifaa vya uchaguzi lakini mara tu uchaguzi
utakapopita kitengo hicho kitahamia katika mji wa Laela.
“Kwahiyo Wakimaliza
uchaguzi wakiandaa ile taarifa tutahakikisha nao wanahamia haa Laela, Watu wa
Fedha na watu wa Utumishi wanawasiliana na watu wa TTCL ili mokongo ule wa
taifa uweze kupatikana hapa Laela na zile huduma zao ziweze kuhamia hapa Laela,
kwa ujumla shughuli zinaenda vizuri na wananchi wanaendelea kuhudumiwa vizuri
hapa Laela,” Alisema.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Apolinari Macheta alisema
kuwa watumishi wa halmashauri hiyo walikuwa wakishiriki usafi wa Jumamosi ya
mwisho wa mwezi katika eneo ambalo halikuwa la kwao na pia walikuwa wakichangia
maendeleo katika maeneo ambao sio ya kwao.
“Tulichelewa sana na ni
maamuzi ambayo yangefanyika hata huko nyuma tungeweza kuwa parefu zaidi lakini
tunakushukuru sana kwa namna mji wetu wa Laela ulivyo hautofautiani na mji wa
sumbawanga na hata kama ni changamoto ni za kawaida haziwezi kufanana na za
wengine kwakweli tunaonekana tuko mjini.” Alisema.
Wakati akitoa neno la
Shukurani mbunge wa jimbo la Kwela Mh. Ignus Malocha alisema kuwa yeye ndio wa
kwanza kutangulia kwani ofisi yake ilikuwa ya kwanza kabla ya Mkurugenzi
kuhamia katika mji huo baada ya wiki mbili tu tangu Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kutoa agizo hilo, hivyo alimshukuru mkuu wa mkoa kwa kusimamia zoezi
hilo la utekelezaji wa agizo la Rais.
No comments:
Post a Comment