Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Chama cha Wananchi (JUVICUF), Hamidu Bobali, akizungumza na waandishi kuhusu hujuma ambazo zinazofanywa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Issa Shing'alang'ata na kulia ni Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Khomein Rwihulla. (Picha na Suleiman Msuya).
NA SULEIMAN MSUYA
MWENYEKITI wa Jumuiya ya
Vijana Chama cha Wananchi (JUVICUF), Hamidu Bobali, amesema hujuma zinazofanywa
na wasimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji kwa
kuwanyima fomu wagombea wa nafasi ya uenyekiti na ujumbe wa vyama vya upinzani ni
ushahidi tosha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinawaogopa wapinzani.
Bobali aliyasema hayo
leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo alibainisha
kuwa mchakato mzima wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea umegubikwa
na hila na hujuma nyingi.
Bobali alisema JUVICUF
imefanya tathmini ambayo imeonesha ushahidi tosha kuwa CCM imeyumba hivyo
inaamini katika figisu na ubabe ambao hauwezi kufanikiwa katika ulimwengu wa
sasa wa uwazi na ukweli.
“Kinachoendelea kwenye
mchakato wa utoaji fomu ni ushahidi kuwa CCM imeyumba, mbaya zaidi
inawezekana Mwenyekiti wa CCM Rais John Magufuli hajui au anadanganywa hivyo wanatumia
mbinu ya kuwanyima wapinzani fomu kumthibitishia chama chake kipo.
Hila tunazofanyiwa CUF
zimepitiliza tunatoa rai kwa Rais Magufuli na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo
wajitokeze na kukemea ukiukwaji wa kanuni unaondelea hatuwezi kuvumilia uonevu
huo tena,” alisema.
Amedai hadi jana
wilayani Liwale mkoani Lindi, wagombea wa vyama vya upinzani hawajapewa fomu huku CCM wakipewa
siku moja kabla ya tarehe ya kuanza, jambo ambalo ni ukiukwaji wa kanuni za
uchaguzi huo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Bobali amedai hali
hiyo imetokea pia wilayani Maswa kata 11 wagombea wao hawajapewa fomu huku jimboni
Mchinga wilayani Lindi msimamizi ametoa maelekezo kwa wasimamizi wasaidizi
wawape daftari tofauti na linalotakiwa kusainiwa na vyama vingine.
“Hali ya Liwale ni
mbaya sana hakuna mgombea wa upinzani amepewa fomu wasimamizi wamefunga ofisi
wiki nzima na hakuna hatua ambazo zimechukuliwa jambo ambalo linaenda kinyume
na kauli za Rais Magufuli anayejiita Rais wa wanyonge sijui wanyonge anawataja
ni wapi kama sio hao wanaochagua viongozi wa mitaa,” alisema.
Mwenyekiti huyo amedai kuwa Rais Magufuli angepaswa kutumia uchaguzi huu kupima chama chake na serikali kwamba
wanakubalika kwa wananchi.
Amedai kauli ya Waziri
Jafo kuwa vyama vya siasa viache kuibua utata ambao unaweza kuharibu uchaguzi
kwa hoja ya kuwa dosari zilizojitokeza ni ndogo Bobali alisema wao hawatoi kauli
tata bali hali halisi ambayo ipo hasa Liwale sio dosari ndogo bali ni kubwa na
wanamtaka waziri kumuondoa msimamizi wa uchaguzi.
No comments:
Post a Comment