Usajili mtandaoni, Tigopesa tayari umeanza
Mbio maarufu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon za
18 zimezinduliwa rasmi leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mh. Dk Harrison Mwakyembe huku akitoa wito kwa watanzania
wajitokeze kwa wingi kushiriki mwakani.
Akizungumza katika hoteli ya Best Western Coral Beach,
Waziri Mwakyembe amewapongeza wadhamini wa Kilimanjaro Marathon wakiongozwa na
Kilimanjaro Premium Lager-42 km, Tigo 21km na Grand Malt 5km kwa kudhamiria
kukuza sekta ya michezo hususani riadha na kufanya mbio hizi kuwa kubwa mwaka
hadi mwaka.
“Inatia moyo sana kuona kuwa
Kilimanjaro Marathon sasa hivi ina washiriki Zaidi ya 11,000 kutoka nchi Zaidi
ya 56 kote duniani. Hili ni jambo zuri sana kwa taifa kwani tunapata fedha za
kigeni kutokana na matumizi yanayofanywa na wageni hawa nchini ikiwemo utalii
ambao sasa hivi tuna kitu kinachojulikana kama sports tourism,” alisema huku
akitoa changamoto kwa watanzania pia wachangamkie fursa ya kufanya utalii wa
ndani baada ya mashindano haya.
Naye Rais wa Chama Cha Riadha Tanzania, Anthony Mtaka, alitoa wito kwa
washiriki wazalendo kuchangamkia zawadi zinazotolewa na Kilimanjaro Marathon
badala ya kukimbilia kushiriki mbio za nje ambazo zawadi zake ni ndogo.
“Ni
vizuri kwenda kupata exposure lakini tusiache zawadi nzuri nyumbani na kufuata
hela ndogo huko nje wakati tunaweza kuzipata hapa,” alisema.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli, alisema tangu mashindano yaanze Kilimanjaro Premium Lager
imewekeza hela nyingi sio tu kusukuma mauzo ambayo wamefanikiwa kwa kiasi
kikubwa, lakini pia kutengeneza ajira na kuchangia uchumi kwa ujumla kupitia
gharama za kuyatangaza,promosheni na masuala mengine ya kimasoko.
“Msimu huu wa Kilimanjaro Marathon pia utakuwa na
faida kubwa kwa wafanyabiashara, sio sisi wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager
tu, bali hata wa chakula, sehemu za kulala wageni, mahoteli na biashara
nyingine,” alisema.
Meneja huyo aliongeza kuwa watatumia fursa hii ya
Kilimanjaro Marathon kutangaza chupa mpya ya Kilimajaro Premium Lager ambayo
ilizinduliwa Juni mwaka huu na ina pamoja na mambo mengine maudhui mbalimbali ya kiafrika (African
pattern) maana bia ya Kilimanjaro inajivunia kupeperusha bendera ya Tanzania.
Naye
Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alisema kampuni yake inajivunia
kudhamini mbio za km 21 kwa mwaka wa tano mfulululizo sasa ambayo ni sehemu ya
mashindno haya ya Kilimanjaro Marathon. “Tunajivunia kuwa sehemu ya tukio hili
kubwa ambalo linawaleta pamoja wanariadha wakubwa na watu mbalimbali kutoka kila sehemu kusherehekea
michezo, burudani, utamaduni, utalii na afya njema.” alisema.
"Natoa wito kwa washiriki
kujisajili kwa kupiga namba *149*20# ili waweze kushiriki katika mbio za
kilometa 21,” alisema na kuongeza kuwa Tigo inashirikiana na makampuni mengine
kudhamini Kilimanjaro Marathon ambayo pamoja na mambo mengine inakuza utalii
pamoja na kuzileta pamoja familia mbalimbali na marafiki kutoka pande zote za
dunia katika kumbukumbu zisizosahaulika.
Naye Mwakilishi wa Grand Malt,
David Tarimo alisema mwaka huu wamejiandaa vizuri na kuwataka washiriki wa
kilometa tano wajiandikishe kwa wingi kwani kutakuwa na Grand Malt za kutosha
na zawadi mbalimbali pamoja na kuwaonesha washiriki kopo lao jipya la 330ml
ambalo lilizinduliwa mwaka huu na linapatikana nchi nzima kwa bei ile ile ya
Tsh 2000. “Grand Malt ambayo ipo kwenye kopo lenye muonekano mzuri zaidi, ni
kinywaji sahihi kwa wanariadha na ni kinywaji ambacho hakina madhara hata kwa
watoto,” alisema.
Wadhamini wengine katika
Kilimanjaro Marathon ni pamoja na Kilimanjaro Water, Barclays Bank, Simba
Cement, TPC Sugar, Precision Air, Kibo Palace Hotel, Garda World Security, Keys
Hotel na CMC Automobiles.
Kwa mujibu ya waandaaji wa
Kilimanjaro Marathon-Wild Frontiers na Executive Solutions, usajili umeshaanza
kwa mtandao kupitia www.kilimanjaromarathon.com. Hadi sasa
waliojisajili ni asilimia 20 zaidi ya idadi ambayo ilikuwa imejisajili muda
kama huu mwaka jana. “Hii ni dalili nzuri kuwa usajili utakuwa mzuri zaidi
msimu huu,” walisema na kuongeza kuwa kutakuwa na usajili Dar es Salaam, Arusha
na Moshi Februari mwakani.
Waandaaji hao pia walitoa wito kwa
washiriki wachangamkie punguzo la bei ambalo lilianza Oktoba Mosi 2019 hadi
Januari 14 , 2020. Kwa raia wa Tanzania na wale kutoka nchi za Afrika Mashariki
watalipa Tsh 15,000 kwa mbio za Km 42 na 21 na Tsh 5000 kwa km 5 lakini kuanzia
Januari 15, 2020 hadi Februari 16, 2020 washiriki watakaojisajili watalipa Tsh
20,000 kwa km 42 na 21 na Tsh 5000 kwa km 5.
Kwa wageni wakazi au wenye vibali
vya kuishi na kufanya kazi na wale wa nchi za SADC watalipa USD 35 kwa km 42 na
21 na USD 5 kwa km 5 kuanzia Octoba 1, 2019 hadi Januari 14, 2020 lakini kuanzia
Januari 15, 2020 hadi Februari 16, 2020 wanaojisajili watalipa USD 45 kwa km 42
na 21 na USD 5 kwa km 5.
Washiriki wa kimataifa watalipa
USD 70 kwa km 42 na 21 na USD 5 kwa km 5 kuanzia Oktoba 1, 2019 hadi Januari
14, 2020 na kuanzia Januari 15 hadi Februari 16, 2020 watalipa USD 85 kwa km 42
na Km 21 na USD 5 kwa km 5.
Kwa mujibu wa waandaaji hao,
usajili utafungwa rasmi saa sita usiku Februari 16, 2020 au pale ambapo idadi
inayotakiwa itatimia.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na
wawakilishi kutoka Chama Cha Riadha Tanzania, Baraza la Michezo Tanzania, Bodi
ya Utalii Tannzania na wadau wengine wa riadha.
Mashindano ya Kilimanjaro Marathon
yanatarajiwa kufanyika Machi 1, 2020 Moshi mjini.
No comments:
Post a Comment