Ofisa Kodi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Julius Mjenga, akiwaelimisha baadhi ya wafanyabiashara wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro leo wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa mikoa ya Morogoro na Pwani. (Picha na TRA).
Na
Veronica Kazimoto, Malinyi
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekutana na
wafanyabiashara pamoja na wananchi wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro kwa
ajili ya kutoa elimu ya kodi ikiwa ni pamoja na kuwasajili wafanyabiashara
wasiokuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi.
Akizungumza na wafanyabiashara hao wakati wa
utoaji wa elimu hiyo, Afisa Kodi Mkuu wa TRA, Julius Mjenga, amewahimiza
kutunza kumbukumbu za biashara zao ili kukadiriwa kodi stahiki.
“Mara nyingi wafanyabiashara wamekuwa
wakilalamika kuwa TRA inawakadiria kodi kubwa lakini mlio wengi hamtunzi
kumbukumbu kwenye daftari linaloonyesha manunuzi na mauzo ya kila siku ili
mwisho wa mwaka Afisa wa Kodi atumie daftari hilo kukukadiria kodi ambayo inaendana
na uhalisia wa biashara yako,” alisema Mjenga.
Mjenga ameongeza kuwa, mfanyabiashara anaetunza
kumbukumbu analipa kodi kidogo ukilinganisha na mfanyabiashara ambaye hatunzi
kabisa kumbukumbu za biashara yake.
Naye mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Samson
Nyanda wa wilayani hapa, ameiomba TRA kutoa elimu ya kodi mara kwa mara kwa
kuwa wafanyabiashara huongezeka kila wakati.
“Elimu hii tuliyoipata ni nzuri mno ila
tunaomba iwe endelevu na ifanyike hata kwa mwaka mara tatu kwa sababu kila
wakati wafanyabiashara wanaongezeka na wengi wao hawana hii elimu ya utunzaji
wa kumbukumbu”, alieleza Nyanda.
Mamlaka ya Mapato Tanzania inafanya Kampeni ya
Elimu, Usajili na Huduma kwa Mlipakodi katika Mikoa ya Morogoro na Pwani ambapo
kwa Mkoa wa Morogoro, timu ya maafisa wa TRA inatarajia kuwafikia
wafanyabiashara na wananchi wa Kilosa, Ulanga, Kilombero, Mvomero, Gairo na
Morogoro vijijini.
Wakati katika Mkoa wa Pwani, timu ya maafisa wa
TRA imelenga kuwafikia wafanyabiashara wote wa maeneo ya Kibaha, Kibiti,
Kisarawe, Mkuranga, Chalinze na Bagamoyo ambapo kampeni hiyo imeanza tarehe 11
na itamalizika tarehe 17 Novemba, 2019.
No comments:
Post a Comment