HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 28, 2019

GCLA KUANZISHA KANZIDATA YA TAIFA YA VINASABA VYA BINADAMU


Na Asha Mwakyonde

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), inatarajia kuanzisha Kanzidata ya Taifa ya Vinasaba vya Binadamu (DNA) lengo likiwa ni kusaidia kwenye utambuzi.

Pia Mamlaka imefuta jumla ya tozo 17, na kupunguza tozo 8 katika utekelezaji wa Sheria ya Kemikali, ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara Tanzania kwa kupunguza mzigo wa gharama kwa wafanya biashara wa kemikali katika uzalishaji  wa bidhaa mbalimbali.


Akizungumza jijini Dar es Salam wakati akielezea mafanikio ya serikali ya awamu ya tano  ya mamlaka hiyo chini ya uongozi wa  Rais John Magufuli katika kipindi cha miaka minne, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice  Mafumiko, alisema kuwa uanzishwaji wa Kanzidata hiyo upo katika hatua za awali ambapo utashirikiana na taasisi mbalimbali za Umma zikiwemo eGA, NIDA na RITA.

Alisema uanzishwaji wa kanzidata itasaidia itasaidia mamlaka kufanya utambuzi wa miili n ahata waliofanya uhalifu.

“Hatufanyi utambuzi kwa miili tu pia hata kwa wanaofanya uhalifu, masuala ya wanyaam hivyo ukiwa na database kwa watu wasiojulikana badala ya kuwaalika ndugu kuangalia ulinganishi tunakwenda kwenye data base kuangalia na kupata ndugu zake,”alisema.

Aliongeza kuwa itasaidia kupambana na uhalifu kwani kuna mambo mengine ya kijinai kama ubakaji, mauaji ya kutumia silaha, mauaji ya albino hivyo itakapoanzishwa kanzidata watuhumiwa watafahamika endapo tu watakuwa kwenye kanzidata.

“Wataalam kutoka katika Taasisi hizo muhimu wameshirikishwa katika hatua za awali za uanzishwaji wa kanzidata ya Taifa hususani utayarishaji wa andiko dhana la uanzishwaji wa kanzidata (concept note),”alisema.


Alisema kwa kuzingatia ushauri wa wataalam katika andiko la uanzishwaji wa Kanzidata ya Taifa ya Vinasaba vya Binadamu (concept note), Mamlaka inakusudia kuanza kuingiza taarifa zinazohusiana na ‘crime and civil index’ kwa kuwa taarifa hizo kuwa zinahitajika katika utambuzi wa binadamu kwa ajili ya utatatuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo uchunguzi wa makosa ya jinai kama vile ubakaji, wizi, mauaji, majanga na masuala ya kijamii yakiwemo mirathi, uhalali wa mzazi kwa mtoto. Alisema mbali na hilo, GCLA inaimarisha ofisi za Kanda kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Dk. Mafumiko alisema Mamlaka inaendelea kuimarisha mahusiano na taasisi zinazotoa huduma za afya hasa katika matibabu ya kisasa yanayohusisha tiba ya "gene therapy", matibabu ya Figo, utambuzi wa jinsi tawala (Sex ambiguity).

“Mamlaka inatarajia kuendeleza Ushirikiano na hospitali ya Muhimbili na hospitali zinginezo katika kuwawezesha wagonjwa wenye matatizo mbalimbali ikiwemo saratani ya damu na mengineyo ambapo tiba yake hufanyika kwa kufanyiwa ‘Bone marrow transplant’.

“Ili kuendelea kufuatilia maendeleo ya wagonjwa baada ya tiba hii, wagonjwa huitajika kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba hususani ‘chimerism’ kwa ajili ya kubaini mafanikio ya transplantation,”alisema.

Alisema vifaa vya kisasa na wataalam waliopo Mamlaka hiyo itaimarisha ushirikiano na Taasisi za kitaaluma mbalimbali ili kuweza kufanya tafiti zinazohusiana na uchunguzi wa vinasaba vya binadamu kwa mfano sickle cell, kisukari, saratani na ‘population genetics’.

“Tafiti hizi zikifanyika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali zitasaidia kuokoa fedha za Umma ambazo zingetumika kwa sampuli kupelekwa nje ya Nchi kwa ajili ya uchunguzi,”alisema.

Aliongeza kuwa inasimamia uingizaji, utumiaji, usambazaji na usafirishaji wa kemikali ambazo ni malighafi za kutengeneza bidhaa mbali mbali viwandani lengo likiwa kuwezesha na kuchangia jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kuelekea uchumi wa Viwanda ifikapo 2025.

Alisema Mamlaka imefanya marekebisho ya Sheria ya Kemikali za Viwandani na Majumbani Namba 3 ya Mwaka 2003 kwa kufanya maboresho ya kifungu cha 43(11) ili kuruhusu uingizaji wa kemikali katika ujazo mkubwa usiokuwa kwenye vifungashio (bulk).

Alisema Mamlaka imenunua Mitambo mikubwa (specialized equipment) yenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa sampuli za dawa za kulevya, vyakula, dawa za binadamu, mifugo, viambata sumu, masalia na viuatilifu, bidhaa za viwandani, uchafuzi wa mazingira, kubaini kiwango cha madini kwenye udongo, kemikali, uchunguzi wa vinasaba yenye thamani ya sh. Bilioni 6.5.

Aliongeza kuwa wamejipanga kuongeza kasi ya upimaji vinasaba ambapo gharama yake ni sh. 300,000 kwa kupima baba, mama pamoja na mtoto na si kama jamii inavyodai gharama sh. 500,000 hadi sh milioni 1.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usimamizi wa Kemikali, Daniel Ndiyo alisema kazi yao ya kitaalamu ambayo hutumia mitambo ambayo hupatikana nje ya nchi, ambapo hulazimika kuagiza watalaamu pindi inapohitaji marekebisho kwakuwa na mikataba funganishi.

No comments:

Post a Comment

Pages